Jeshi la Nigeria limethibitisha kifo cha Meja Jenerali mstaafu Rabe Abubakar, aliyekuwa msemaji wa jeshi kati ya mwaka 2015 na 2017, baada ya kufariki akiwa mikononi mwa watekaji nyara waliomteka mwezi uliopita katika jimbo la Katsina, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Abubakar alitekwa pamoja na mkewe walipokuwa wakisafiri katika eneo hilo, huku kundi lililohusika na utekaji huo likiwa bado halijajitokeza wala kutambulika rasmi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna wa Usalama na Masuala ya Ndani wa Jimbo la Katsina, Nasiru Mu’azu, alisema jenerali huyo alifariki kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimsumbua, ikiwemo ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, licha ya juhudi zilizofanywa na serikali na vyombo vya usalama kuhakikisha anaokolewa salama.
Kifo hicho kimeibua tena hofu kuhusu hali ya usalama katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Nigeria, ambako makundi ya wahalifu wanaojulikana kama majambazi yamekuwa yakihusishwa na matukio ya utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia, wizi wa mifugo na mashambulizi dhidi ya wananchi.
Wakati huo huo, familia ya marehemu imetoa wito kwa mamlaka za usalama kuongeza juhudi za kumuokoa mke wa jenerali huyo ambaye bado anashikiliwa na watekaji nyara.
Kifo cha Meja Jenerali Abubakar kinatajwa kuwa pigo kubwa kwa taifa la Nigeria na sekta ya ulinzi, kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa akiwa jeshini kabla ya kustaafu.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime