Siku ya Wanawake Duniani

Kila mwaka Machi 08, Umoja wa Mataifa husheherekea haki zilizopatikana kwa bidii za wanawake- na kuangazia changamoto ambazo bado ziko mbele katika kukomesha ubaguzi wa kijinsia katika karibu nyanja zote za maisha.

"Usawa wa kijinsia wa leo, kesho na endelevu" ndio kauli mbiu ambayo Umoja wa Mataifa umeichagua mwaka huu kuadhimisha kile kinachojulikana rasmi kama Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Dkt Maxime Houinato, mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, aliiambia BBC kwamba "kukuza usawa wa kijinsia katika mazingira ya mzozo wa mabadiliko ya tabia nchi na upunguzaji wa hatari ya majanga ni mojawapo ya changamoto kubwa duniani kwa karne ya 21".

"Wanawake na wasichana wanapitia athari kubwa zaidi za mabadiliko ya tabia nchi," aliongeza.

Kwa kweli, utafiti wa Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa wanawake na wasichana hufa kwa idadi kubwa katika majanga ya asili.

"Kwa mfano, asilimia 95 ya waliofariki katika mafuriko ya visiwa vya Solomon 2014 walikuwa wanawake, 55% ya waliofariki katika tetemeko la ardhi la 2015 nchini Nepal walikuwa wanawake na 59% ya waliokimbia makazi yao kufuatia Kimbunga Idai mwaka 2019 nchini Malawi walikuwa wanawake," UN Women imesema kwenye tovuti yake

Zaidi ya hayo, majanga yanayohusiana na hali ya hewa yamezidisha matatizo ya kijamii na kiuchumi.

"Nchini Uganda, kwa mfano, upotevu wa mifugo, upungufu wa mazao, na ukosefu wa chakula kutokana na ukame uliokithiri, na uvamizi wa nzige ulibainika kuongeza idadi ya wanafunzi walioacha shule, kulazimisha wasichana kufanya kazi zaidi , na kuongeza matukio ya ndoa za utotoni kwa kubadilishana kwa chakula," makala katika wakala wa habari unaolenga maendeleo, Inter Press Service, inaeleza.

Zetkin alijumuika na wanawake 100 kutoka nchi 17 katika Kongamano la Kimataifa la Wanawake Wanaofanya Kazi katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen mwaka 1910.

Mkutano huo kwa kauli moja ulikubaliana na pendekezo la Zetkin kwamba kuanzia mwaka unaofuata Siku ya Wanawake itaadhimishwa nchini Austria, Denmark, Ujerumani na Uswizi.


Wazo la Zetkin la Siku ya Kimataifa ya Wanawake halikuwa na tarehe maalum.

Ilirasimishwa baada ya mgomo wa baada ya vita, wanawake nchini Urusi mwaka 1917. Wanawake walidai "mkate na amani" - na siku nne za mgomo wa wanawake, Tsar alilazimika kujiuzulu na serikali ya muda hiyo iliwapa wanawake haki ya kupiga kura.

Tarehe ambayo mgomo wa wanawake ulianza kwa kalenda ya Juliana, ambayo wakati huo ilikuwa ikitumika nchini Urusi, ilikuwa Jumapili Februari, 23.

Siku hii katika kalenda ya Gregori ilikuwa Machi 8. Huu ndio wakati ambapo sasa inaadhimishwa kama siku ya mapumziko nchini Urusi na nchi zingine takribani dazeni mbili.


Siku ya wanawake duniani inaadhimishwa kama sikukuu ya umma katika nchi saba za Afrika. Hii ni pamoja na Eritrea, katika kutambua mchango mkubwa ambao wanawake na wasichana walitoa - kama wapiganaji - katika mapambano ya muongo mzima ya uhuru wa nchi hiyo.

Mataifa mengine ya Afrika ambayo yametangaza tarehe 8 Machi kuwa siku ya mapumziko ni Angola, Burkina Faso, Guinea-Bissau, Sierra Leone ,Uganda na Zambia.

Huko Madagascar, ni siku ya mapumziko kwa kwa wanawake pekee.

Baadhi ya nchi za Kiafrika zina Siku yao ya Wanawake - Afrika Kusini inaadhimisha kama siku ya mapumziko tarehe 9 Agosti kwa heshima ya wanawake 20,000 walioandamana siku hiyo mwaka 1956 kupinga sera za kibaguzi ya utawala wa wazungu wachache uliokuwa madarakani kwa wakati huo.

"Unampambana na mwanamke, unagonga mwamba," wanawake hao waliimba huku wakielekea kwenye kiti cha mamlaka ya serikali katika mji mkuu wa Pretoria.

Mbali na hayo, Umoja wa Afrika umetangaza tarehe 31 Julai kuwa Siku ya Wanawake wa Afrika.

AU inasema siku hiyo inalenga "kutambua na kuthibitisha" nafasi ya wanawake katika "kufikia uhuru wa kisiasa wa Afrika na kuendeleza hali ya kijamii na kiuchumi ya wanawake katika bara hilo".

Ingawa bado kuna mengi yanahitajika kufanywa ili kufikia usawa wa kijinsia.

Wanawake barani Afrika wamepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2021 zinaonesha kuwa Rwanda ina idadi kubwa ya wanawake bungeni - 61%, ikifuatiwa na Cuba na Bolivia zenye 53% kila moja na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa 50%.

Afrika Mashariki na Kusini ndizo zenye uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake bungeni katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara - 32% kufikia Disemba 2020, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa 24.5%.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii