Nchini Senegal, mashabiki watatu katika kundi la kwanza waliokamatwa nchini Morocco kufuatia vurugu wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON huko Rabat walitua uwanja wa ndege wa Dakar jana usiku, wakilakiwa kama mashujaa na umati wa mashabiki baada ya miezi mitatu gerezani.
Umati wa watu ulionyesha furaha yao wakati mashabiki hao watatu, Abdoulaye Dieng, Ibrahima Diop, na Aziz Wade, walipovuka mlango wa uwanja wa ndege. Zaidi ya mia moja ya wenzao kutoka Gaïndé ya 12 (kamati kuu ya madhabiki wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Senegal) walikuwepo. Bendera za Senegal zilipeperushwa juu ya umati mdogo, na kila mtu alitaka kuzikumbatia, kuzibeba.
Coumbe Thiaw, aliyetoka Saly, akiwa amevaa kofia ya kijani, njano, na nyekundu, alitabasamu kwa furaha: "Ni faraja kubwa. Tunafurahi sana kwa sababu imekuwa miezi mitatu tangu hatujawaona ndugu zetu." Gaïndé ya 12 ni familia; ukimgusa mtu mmoja, unagusa familia nzima.
Kwa tukio hilo, djembe na tarumbeta husikika. Abdoulaye Dieng, kutoka eneo la Richard-Toll, kaskazini mwa Senegal, hawezi kuacha kutabasamu baada ya miezi mitatu akiwa mbali na nchi yake: "Sasa, tunasema al-hamdu lillah, kwa sababu tumerudi tuko salama salimi, na mradi tu tuko salama, kuna matumaini."