Ukraine imesema kwa sasa iko tayari kuanza tena usambazaji wa mafuta ya Urusi kuelekea Ulaya baada ya kukamilisha ukarabati wa bomba la mafuta la Druzhba ambalo liliharibiwa mwezi Januari kufuatia shambulio la Urusi.
Serikali mjini Kyiv imesema inaweza kuanza tena kusafirisha mafuta hayo ikiwa itapokea ombi rasmi, huku ikitumai kuwa hatua hiyo itapiga jeki mpango wa kupewa mkopo wa mamilioni ya euro kutoka Umoja wa Ulaya.
Bomba hilo la Druzhba limekuwa kitovu cha mzozo kati ya Hungary na Slovakia, ambazo zimekuwa zikiilaumu Kyiv kwa kuchelewesha makusudi ukarabati huo. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametahadharisha kuwa vikosi vya Urusi vinaweza kulishambulia tena bomba hilo.