Bidhaa ambazo zitaguswa na jinsi Afrika itakavyoathirika.

Huku uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ukiendelea, athari za kiuchumi kutokana na vita vinavyoendelea tayari zimeanza kujitokeza kote ulimwenguni na Afrika hazijaachwa nyuma.

Mwandishi wa Habari za Biashara wa BBC Afrika Victor Kiprop anaeleza.

Nchi hizo mbili (Urusi na Ukraine) ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa bidhaa kuu zikiwemo mafuta na gesi, ngano na mafuta ya alizeti, ikimaanisha kwamba usumbufu wowote wa usambazaji unaweza kuleta msukosuko katika uchumi wa dunia.

Kampuni kubwa zaidi duniani za meli za Maersk , CMA CGM zimesitisha utoaji wa majani Chai kutoka Mnada wa Chai wa Mombasa hadi bandari za Urusi na Ukraine.

Kwa mujibu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Chai Afrika Mashariki (EATTA), ambao ndio mnada mkubwa zaidi wa chai duniani, kampuni za meli zimetaja ukosefu wa usalama na sasa zinawashauri wafanyabiashara kutafuta bandari mbadala za kupokea bidhaa hiyo huko Ulaya.

Hii sasa inasababisha vichwa kuuma kwa wafanyabiashara kwani watalazimika kuingia gharama za ziada kuhamisha shehena za bidhaa hiyo kufika sehemu ya mwisho iliyopangwa.

Urusi inachangia takriban 5% ya mauzo ya chai kutoka Kenya na ni miongoni mwa maeneo matano ambayo yanachangia 75% ya mauzo ya chai duniani kote.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa EATTA, Edward Mudibo, anasema "Tunatarajia ucheleweshaji wa kumaliza mauzo na kwa kuzingatia kuwa mfumo wa malipo wa SWIFT pia ni miongoni mwa vikwazo vilivyowekewa Urusi, hivi karibuni wafanyabiashara hawataweza kufanya malipo.

Mgogoro huo ukiendelea kwa mwezi mwingine mmoja, hatutaweza kuuza nje chai nje ya nchi."

Bw. Mudibo anatarajia kupungua kwa mahitaji ya chai ya Kenya katika siku za usoni- na hii itatafsiri kuwa bei ya chini, hivyo basi hasara, ingawa takwimu kamili haziko wazi kwa sasa.

Licha ya uamuzi wa Jumanne wa nchi tajiri kwa mafuta kutoa mapipa milioni 60 ya mafuta kutoka kwa hifadhi zao za kimkakati ili kutuliza hofu ya uhaba wa usambazaji, bei ya mafuta imeendelea kupanda, ikifikia dola 110 kwa pipa siku ya Jumatano.

Barani Afrika, nchi kadhaa tayari zimerekodi ongezeko la bei ya mafuta lawama ikirushiwa kukatika kwa mzunguko ya ugavi unaohusishwa na mzozo wa Urusi na Ukraine.

Siku ya Jumanne, Wakala wa Udhibiti wa Petroli wa Sierra Leone (PRA) ulitangaza ongezeko la $0.17 katika bei ya pampu ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Nchini Zambia, bei ya lita moja ya petroli ilipanda kwa dola 0.12 na dizeli kwa dola 0.15, huku mafuta ya taa yakiendelea bila kubadilika.

Hali si tofauti nchini Afrika Kusini ambapo lita moja ya petroli sasa inagharimu dola 0.095 zaidi na nchini Tanzania ambapo sasa itagharimu zaidi ya dola 1.10, licha ya uamuzi wa Jumatatu wa serikali kufuta tozo ya mafuta ya $0.043.

Nchi ambazo hazina mifumo ya udhibiti wa bei ndizo zinazohisi athari kwa haraka kwa kuzingatia gharama ya mafuta yao.

Patrick Obath, Mchambuzi huru wa Mafuta kutoka Kenya anasema "Athari za kudorora zinaweza pia kuonekana katika bei ya bidhaa zingine ambazo huenda zikapanda kutokana na hilo".

Nchi kama vile Kenya ambako serikali inadhibiti bei ya bidhaa za mafuta huenda zisipate athari yake mara moja. (Kenya ina hazina ya uimarishaji wa mafuta ambayo serikali hutumia kukabiliana na ongezeko la bei katika bei ghafi za kimataifa ili kuweka bei katika kiwango kinachohitajika)

Bei za vyakula tayari zimekuwa zikipanda kutoka mwaka 2021 kote ulimwenguni kutokana na kutatizika kwa usambazaji kulikosababishwa na Covid-19, hali ambayo inaweza kuwa mbaya zaidi ikiwa usafirishaji wa chakula kutoka Urusi na Ukraine utatatizwa na vita.

Nchi hizo mbili ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa bidhaa kuu zikiwemo mafuta na gesi, ngano na mafuta ya alizeti, ikimaanisha kwamba usumbufu wowote wa usambazaji unaweza kuleta msukosuko wa kiuchumi duniani.

Ngano, ambayo Urusi na Ukraine hutoa karibu 30% ya pato la kimataifa, imekuwa janga kubwa zaidi.

Siku ya Jumanne, bei ya ngano ilipanda hadi kiwango cha juu zaidi kilichoonekana tangu mwaka 2008, jambo ambalo kuna uwezekano wa kuzikumba nchi zinazotegemea uagizaji bidhaa ikiwa ni pamoja na Misri.

Kulingana na Mamlaka Kuu ya Bidhaa za Ugavi ya Misri (GASC) Urusi ilitoa takriban 50% ya ngano iliyoagizwa nchini Misri mwaka 2021, wakati Ukraine ilikidhi asilimia 30 ya mahitaji ya nafaka nchini humo.

Misri sasa inabidi kutafuta usambazaji wake kutoka maeneo mbadala, lakini inaweza isitoshe kukidhi mahitaji ya juu ya uagizaji wa bidhaa hiyo nchini humo, kumaanisha kwamba bei za bidhaa kuu zinaweza kupanda zaidi, na kubana mapato ya kaya katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Ongezeko la jumla la bei za vyakula duniani linatarajiwa kutatizwa zaidi kutokana na uhaba wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea.

Nchini Kenya ambapo bei ya mbolea imekuwa ikipanda kwa kasi tangu mapema mwaka jana, serikali sasa inaonya kwamba bei ya mfuko wa kilo 50 wa mbolea inaweza kufikia dola 61.5 kutoka $35.05 mapema mwaka jana. "Kutokana na hali ilivyo sasa hivi, bei zinaweza kupanda zaidi. Ikiwa hali hii itaendelea, bei ya mbolea ya DAP, inaweza kufikia shilingi 70000 kwa mfuko, Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya alisema Jumanne.

Kando na ngano na mahindi, mafuta ya alizeti yanasalia kuwa moja ya bidhaa kuu za kilimo kutoka Ukraine hadi Afrika.

Misri kwa mfano inategemea Ukraine na Urusi kwa sehemu kubwa ya mafuta yake ya alizeti na changamoto yoyote inaweza kusababisha bei ya mafuta ya kupikia ikapanda na kuongeza shinikizo lililopo kwa bei za vyakula nchini.

Kutokuwa na uhakika kuhusu usambazaji wa mafuta ya alizeti tayari kumesababisha mahitaji ya mafuta mengine ya kula kama vile mawese kupanda sana kama mbadala ya yao.

Hii ni nafasi kwa nchi kama Nigeria kuchukua fursa ya uhaba wa usambazaji kwenye soko.

Mnamo mwaka 2020, tani milioni 73 za mafuta ya mawese zilitumiwa duniani kote, lakini Nigeria ilichangia tani milioni 1.2 tu au 2% tu katika Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii