Jeshi la Marekani limesema linaanza leo Jumatatu kuweka vizuizi kwa bandari zote za Iran.
Vizuizi hivyo ni pamoja na usafirishaji mafuta ya nchi hiyo baada ya mazungumzo ya amani yaliyofanyika Pakistan kuvunjika na kila upande kuulaumu mwingine.
Tangazo hilo limetolewa licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha vita kwa muda wa wiki mbili yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili ili kutoa nafasi ya mazungumzo.
Kamandi ya Jeshi la Marekani yenye jukumu la operesheni za kanda ya Mashariki ya Kati imesema vizuizi hivyo vinazilenga meli za mataifa yote zinazoingia na kutoka kwenye bandari za Iran na maeneo yote ya mwambao wa nchi hiyo.
Kamandi hiyo imesema operesheni hiyo haitazihusu meli zinatopita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz kuelekea mataifa mengine ya eneo la Ghuba. Mazungumzo kati ya Iran na Marekani yalimalizika hapo jana bila makubaliano na kwa Washington kuituhumu Iran kukataa kuachana na mpango wake wa nyuklia.