Msanii mkongwe wa Dancehall kutoka Kenya, Redsan, ametangaza rasmi tamasha lake kubwa litakalofanyika baadaye mwaka huu, akilenga kuandika historia mpya katika muziki wa Afrika Mashariki.
Tangazo hili linakuja muda mfupi baada ya mafanikio makubwa ya show ya Nyashinski, ambayo ilivuta hisia za mashabiki wengi na kuthibitisha kuwa muziki wa Kenya unaendelea kukua kwa kasi na kupata heshima kubwa ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Kupitia taarifa yake rasmi, Redsan ametambulisha tamasha lake lijulikanalo kama “Redsan At 30”, ambalo linatarajiwa kufanyika tarehe 29 Agosti 2026 katika ukumbi maarufu wa Carnivore Grounds uliopo jijini Nairobi. Tamasha hili lina lengo la kusherehekea miaka 30 ya Redsan ndani ya muziki, safari iliyojaa mafanikio, changamoto na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa Dancehall Afrika.
Redsan, anayejulikana kwa vibao vingi vilivyotikisa ukanda wa Afrika Mashariki, ameahidi kuwa show hiyo itakuwa ya kipekee na ya kukumbukwa, ikiwa na burudani ya hali ya juu, wageni maalum, pamoja na maonesho yatakayobeba historia nzima ya kazi yake.
Mashabiki wa Dancehall tayari wameanza kuonyesha hamasa kubwa mitandaoni, wakisubiri kwa hamu kuona namna ambavyo “Dancehall King” huyo atakavyofunga safari yake ya miaka 30 kwa kishindo.
Kwa ujumla, mwaka 2026 unaonekana kuwa wa kipekee kwa muziki wa Kenya, huku wasanii wakubwa wakizidi kuandaa matamasha makubwa yanayoinua tasnia hiyo katika ramani ya kimataifa. Tamasha la Redsan linaonekana kuwa moja ya matukio yatakayovuta hisia na kukusanya mashabiki kutoka pande mbalimbali za Afrika na dunia kwa ujumla.