Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo ametangaza neema kwa wakulima wa Idofi, Wilaya ya Makambako, ambapo Serikai inaenda kutekeleza mradi Mkubwa wa Umwagiliaji utakaonufaisha ekari zaidi ya 1.300.
Amesema, hatua hiyo itainua uchumi hivyo ni muhimu kuunga mkono mpango wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji katika skimu ya Idofi, utakaowezesha kilimo chenye tija na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo katika eneo hilo.
Mhe. Chongolo amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Idofi.
Amesema, Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanatumia kikamilifu rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo endelevu.
“Nimekuja mwenyewe kuwaambia ukweli wa kile kinachotakiwa kufanyika. Ni lazima tukae mkao wa watu tunaojua tunachokitaka,” amesisitiza Waziri Chongolo.
Mheshimiwa Chongolo, amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya kilimo, kwa lengo la kuinua uchumi wa wanachi.
Ameongeza kuwa, alibaini kuwa wananchi wengi hawalimi kwa tija licha ya kuwa na maeneo makubwa, kutokana na changamoto ya maji na miundombinu duni ya kilimo.
“Wataalamu walibaini kuwa eneo linalolimwa kwa sasa halifiki ekari 300, wakati eneo lote lina ukubwa wa ekari 1,300. Likiboreshwa, wananchi wataweza kulima eneo lote kwa tija na kuinua uchumi hii ni fursa kwetu wanachi wa Makambako,”alieleza.
Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya wataalamu, mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji na uwekaji wa miundombinu ya kisasa itakayowezesha uzalishaji wa mazao mwaka mzima.
Aidha Waziri Chongolo amewahakikishia wananchi kuwa hakuna mkulima atakayepoteza eneo lake kutokana na utekelezaji wa mradi huo.
“Eneo litakapoboreshwa, hakuna mkulima atakayeondolewa. Wanaolima sasa ndiyo watakaobaki, isipokuwa mtu aamue mwenyewe kuondoka au kuuza eneo lake,” amesisitiza.
Hata hivyo, amewahimiza wananchi kuwa tayari kushirikiana na Serikali kwa kutoa nafasi kwa muda mfupi ili kuruhusu utekelezaji wa mradi, kabla ya kurejeshwa katika maeneo yao kwa manufaa makubwa zaidi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Makambako, Kenneth Haule, amewahimiza wananchi kujifunza kutoka katika maeneo ambayo tayari yamenufaika na miradi ya Umwagiliaji kama vile Igomelo, Pawaga na Itipingi, ambako uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Usanifu Mhandisi Sadati Kolowa kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji amebainisha kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni kipaumbele katika miradi yote ya Umwagiliaji, kuanzia hatua za awali hadi utekelezaji wake, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa na maridhiano ya pamoja.
Naye Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema, amesema wananchi watapewa umiliki wa maeneo yao ndani ya mradi huo na watakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi juu ya matumizi ya ardhi zao.
Mwema, ameongeza kuwa kwakuwa utekelezaji wa mradi utajumuisha maboresho mbali mbali ndani ya eneo hilo, shughuli zote za maboresho zitahusisha wananchi wenyemashamba ndani ya eneo la mradi na hakuna uharibifu wa mazao utakaofanyika na wala hakuna nguvu itakayotumika kuhamisha wanachi kwani watapanga na kuamua wao wenyewe
Kwa niaba ya wananchi, mkulima wa eneo hilo Erasto Mbuna, ameomba Serikali kupitia wataalamu kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu na kuzingatia maoni yao katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi.
Mradi wa Umwagiliaji Idofi unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo, ukiwa sehemu ya mkakati wa Serikali kwa kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa, chenye tija na kinachochangia kwa kasi ukuaji wa uchumi wa wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.