Waziri Mkuu wa Kanada, Mark Carney, amesema hawezi kuondosha uwezekano wa nchi yake kushiriki kijeshi dhidi ya Iran kwenye vita vinavyoendelea kwenye eneo la Mashariki ya Kati.
Ziara yake ya wiki hii nchini Australia imetandwa na vita hivyo vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, hasa baada ya kiongozi huyo wa Kanada kunukuliwa wiki chache nyuma akipingana na kile alichokiita kupasuka kwa "utawala wa dunia unaoelemea upande mmoja."
Akizungumza akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Anthony Albanese mjini Canberra, alisema nchi yake "itasimama na washirika wake na daima itawalinda raia wa Kanada."
Hata hivyo, Carney alikiri kuwa mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yalikuwa kinyume na sheria za kimataifa.
Lakini alisema anaunga mkono juhudi za kuizuwia Tehran isiwe na silaha za nyuklia, huku akitowa wito kwa pande zote kuweka silaha chini.