China imejitolea kuwa mpatanishi kwenye mzozo wa sasa wa Mashariki ya Kati baada ya uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran kusababisha vita kusambaa kote kwenye eneo hilo.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China imesema kwenye taarifa yake kwamba "Beijing iko tayari kuwa mpatanishi kati ya pande zinazozozana" kwa sasa.
Hata hivyo, China ni mshirika wa karibu wa Iran na imeshasema tangu awali kwamba inaiunga mkono Tehran kwenye kulinda mamlaka yake, huku ikizitaka Marekani na Israel kusitisha mashambulizi yao.
Hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ametowa maneno makali dhidi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, wakati wa mazungumzo yao kwa njia ya simu.
Al Thani amemuambia Araghchi kuwa Tehran inajaribu kuwaingiza majirani zake vitani.
Iran imekuwa ikiyashambulia maslahi na vituo vya Marekani kwenye mataifa ya Ghuba tangu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi yake mwishoni mwa wiki iliyopita.