DCEA Yakamata Tani 9.93 za Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 9.93 za dawa za kulevya pamoja na chupa 1,795 za dawa tiba mbalimbali katika operesheni zilizofanyika Januari na Februari 2026.

Aidha operesheni hizo zilisababisha kukamatwa kwa watuhumiwa 151, magari sita na pikipiki 29, huku ekari 87.5 za mashamba ya bangi zikiteketezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika Kituo cha Forodha cha Mutukula, maofisa walinasa shehena ya dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine, Morphine na Fentanyl zilizokuwa zinasafirishwa kwa basi la abiria la SR Classic kutoka Uganda.

Watuhumiwa saba walikamatwa kuhusika na tukio hilo, akiwemo Hassan Omary Mwambashi maarufu Macheni na Ibrahim Saidi Malindi.

Aidha, kiasi kikubwa cha bangi aina ya skanka kilikamatwa, ikiwemo kilogramu 81.883 zilizofichwa kwenye lori la apples jijini Dar es Salaam na kilogramu 488.64 zilizopatikana Chanika Buyuni.

Operesheni nyingine mkoani Mbeya na Arusha pia zilisababisha kukamatwa kwa wasafirishaji wa skanka na mirungi.

DCEA imesisitiza kuwa matumizi holela ya dawa tiba aina ya opioids ni hatari, kwani yanaweza kusababisha uraibu na hata vifo vya haraka.

Hata hivyo serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na wananchi ili kuziba mianya ya uchepushaji wa dawa na kutokomeza biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii