Office of Foreign Assets Control (OFAC) ya Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya jeshi la Rwanda na maofisa wake wanne wakuu, kwa madai ya kutoa usaidizi wa moja kwa moja wa kijeshi kwa waasi wa M23 na washirika wao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Thomas Pigott, amesema mchakato wa kujadili vikwazo hivyo ulichukua takriban miezi miwili kabla ya kufikia hatua ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa Pigott, hatua hiyo inahusisha kufungiwa kwa mali zote zilizopo nchini Marekani pamoja na marufuku ya miamala yoyote kati ya wahusika hao na raia au makampuni ya Marekani, isipokuwa kwa mikataba au shughuli zilizokuwa tayari zinaendelea hadi Aprili 1, 2026.
Aidha, Pigott ameeleza kuwa siku chache baada ya kusainiwa kwa tamko linalohusiana na Makubaliano ya Washington, wapiganaji wa AFC/M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda walichukua udhibiti wa mji wa Uvira, akitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano hayo.
Hata hivyo amesisitiza kuwa M23 tayari ni kundi lililowekewa vikwazo na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa (UN).