Madereva watano wa ‘Ambulance’ matatani kwa kupakia abiria

Madereva watano wa magari ya kubebeba wagonjwa (Ambulance) wamekamatwa na polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kubeba abiria kutoka Dar es salaam kuelekea Mtukula mkoani Kagera.

Akizungumza na waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro SACP Alex Mkama amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika oparesheni kabambe ya kulinda usalama kwa watumiaji wote wa Barabara inayolenga kuzuia ajali kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka iliyoanza Desemba mosi mwaka 2025.

Kamanda Mkama anawataja waliokamatwa kuwa ni George Mung’ongo (29) mkazi wa Arusha aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 933 EPL aina ya Toyota Land Cruiser D/L namba 4004926724 ambayo ilikuwa na abiria 8.

Anawataja wengine kuwa ni Paul Zacharia (37) aliyekuwa akiendesha gari lenye namba T 927 EPL aina ya Toyota Land Cruiser D/L namba 4001696044 akiwa na abiria 9 na Victor Baroho (30) akiendesha gari lenye namba T943 EPL aina ya Toyota Land Cruiser D/L namba 4006405108 iliyobeba abiria 9, madereva hao wote ni wakazi wa Dar es salaam.

Kamanda Mkama anawataja watuhumiwa wengine kuwa ni Godliving Sawe (37) akiwa na abiria 12 kwenye gari namba UA 055 BP aina ya Toyota Hiace D/L namba 4000229499 na John Masae (26) akiwa na abiria 5 kwenye gari lenye namba za usajili T 988 EPL Toyota Land Cruiser madereva hao wote wakiwa ni wakazi wa Dar es salaam.

Akizungumzia tukio hilo Shamim Abdalah mkazi wa Morogoro amesikitishwa na kitendo cha madereva hao kutumia magari ya wagonjwa kama mabasi na kujipatia kipato kwa manufaa yao binafsi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“matumizi mabaya ya magari ya wagonjwa yanaweza kusababisha wagonjwa kukosa huduma kwa wakati na hata wazazi waliopaswa kuwahishwa kwenye hospitali kubwa kupata huduma muhimu za kujifungua wanaweza kutishia uhai wao” amesema Shamim.

Hivyo Shamim ameipongeza serikali kwa jitihada za kuwakamata madereva hao na kuiomba kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hizo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii