Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameshiriki katika Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliofunguliwa rasmi Novemba 24 mwaka huu jijini Luanda, Angola na kuwashirkikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi za Afrika na Umoja wa Ulaya.
Mhe. Dkt. Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano huo ambao umefunguliwa kwa pamoja na Wenyeviti Wenza, Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mhe. João Lourenço na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Mhe. Ursula von der Leyen.
Awali akizungumza kwenye Mkutano huo, Mhe. Ursula amesema kuwa umefika wakati kwa Jumuiya hizi mbili kuimarisha zaidi ushirikiano kuliko hapo awali ili kuwawezesha waanchi katika Jumuiya hizi muhimu kunufaika zaidi na ushirikiano huo hususan kwenye sekta muhimu kama vile biashara, uwekezaji, miundombinu, teknolojia na nishati safi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya unatakiwa kutoa majibu chanya kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jumuiya hizi hususan Waafrika kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana na ukosefu wa nishati safi na kwamba Umoja wa Ulaya upo tayari kushirikiana na Afrika ili kutatua changamoto hizo kwa kuleta ujuzi mpya na fursa mpya za biashara.
Kuhusu nishati safi, Mhe. Ursula amesema EU kupitia Mpango wa “Scaling Up Renewables in Africa” umekusanya Euro bilioni 15.5 kwa ajili ya kufadhili miradi ya nishati safi Barani Afrika huku akisisitiza kuwa kila Bara linatakiwa kufurahia upatikanaji wa nishati safi kwa bei nafuu.
Kwa upande wake, Mhe. Rais João Lourenço amesitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kama njia ya kukuza uhusiano bora kati ya Afrika na Ulaya, akifafanua kuwa amani na ushirikiano wa kiuchumi ni misingi muhimu inayoweza kuleta ustawi wa pamoja kwa mabara yote mawili.
Vilevile alitoa wito kwa mataifa ya Afrika na Umoja wa Ulaya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, hususan katika maeneo ya maendeleo na biashara
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime