Watu 94 wamefariki dunia kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwenye mji wa mlimani wa Petropolis nchini Brazil. Mvua hizo zilizoanza kunyesha siku ya Jumanne zimesababisha maporomoko ya udongo yaliyofunika nyumba na mafuriko yaliyosomba magari na mabasi. Meya wa mji huo Rubens Bomtempo ameonya kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka. Idara ya zimamoto na vikosi vya uokoaji vinaendelea na zoezi la kuwatafuta waathirika. Takriban nyumba 80 zinasemekana kuathiriwa na maporomoko ya udongo na zaidi ya watu 377 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Rais wa Brazil Jair Bolsonaro, ambaye yuko Moscow amezungumza na mawaziri kutoa msaada wa haraka kwa wahanga. Tangu mwezi Desemba, mvua kubwa zimesababisha mafuriko na maporomoko ya udongo huko Kaskazini Mashariki mwa Brazil na katika jimbo la Sao Paulo