Mwalimu Aliyebaka Wanafunzi 13, Kutunga Mimba 8 Ahukumiwa Kifungo cha Maisha Jela.

Mwalimu mmoja wa dini nchini Indonesia, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kuwabaka wanafunzi 13 wa kike.
Herry Wirawan, ambaye alikuwa mmiliki na mwalimu wa dini ya Kiislamu katika shule hiyo ya bweni, alikabidhiwa adhabu hiyo siku ya Jumanne, Februari 15.
Kulingana na ripoti ya polisi, wanane kati ya wanafunzi hao waliobakwa ni walio na umri wa kati ya miaka 12 hadi 16 na wote ni wajawazito
Wirawan, alituhumiwa kuwanyanyasa kingono wanafunzi hao na kuwajeruhi vibaya baadhi yao.
Mienendo chafu ya Wirawan iligunduliwa mnamo Mei 2020, baada ya mzazi wa mmoja wa msichana walioathiriwa kuzua kwamba mwanawe ni mjamzito.Inaripotiwa kwamba alitenda uhalifu huo kati ya mwaka 2016 na 2021.
Viongozi wa mashtaka walimtaka mwalimu huyo kuhukumiwa kifo ama hata kuchinjwa kwa sababu ya madhara aliyosababishia watoto hao.
Serikali ya taifa hilo pia imeahidi kwamba itawalipa kila msichana aliyeathirika KSh681,600 kama fidia.
Afungwa jela miaka 20 kwa kumbaka na kuua mtoto wa chekechea
Katika kisa sawia na hicho, mwanamume mmoja huko Maragua, Kaunti ya Murang’a amesukumwa jela miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi na kumuua mwanafunzi wa shule ya chekechea mwenye umri wa miaka 5.
Isaak Mwangi Wakanyi, 46, alishtakiwa kwa kumteka nyara mtoto huyo alipokuwa akitoka shuleni Septemba 5, 2013 kabla ya kutekeleza vitendo hivyo vya kinyama.
Kulingana na mashahidi, mwili wa mtoto huyo ulipatikana umetupwa kando ya barabara na wanafunzi wakielekea shuleni asubuhi iliyofuata.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii