Uchaguzi wa urais Côte d'Ivoire Kampeni zaanza

Kampeni za uchaguzi nchini Côte d'Ivoire zinaanza leo Ijumaa, Oktoba 10. Uchaguzi wa urais utafanyika Jumamosi, Oktoba 25. Kabla ya hapo, kwa muda wa wiki mbili, wagombea watano walioidhinishwa na Baraza la Katiba watajaribu kuwashawishi wapiga kura.

Mikutano ya hadhara, misafara, na mikutano na makundi madogo ya kijamii: Jean-Louis Billon anaanza kampeni yake kwa gwaride katika wilaya ya Abidjan ya Koumassi. Kisha atafanya mkutano huko Marcory, wilaya nyingine katika mji mkuu wa kiuchumi wa Côte d'Ivoire, inayoongozwa na Meya Aby Raoul wa Chama PDCI-RDA. Kwa Jean-Louis Billon, changamoto ni kuwashawishi wapiga kura wa chama chake cha awali, PDCI, kumuunga mkono. Chama hiki bado hakijatoa maagizo yoyote ya kupiga kura, kufuatia kukataliwa kwa kiongozi wake, Tidjane Thiam, kugombea. "Upinzani wa kwanza unapatikana ndani ya chama chake," wanasisitiza wale walio karibu naye, ambao wanaendelea kuwa na matumaini, wakitoa mfano wa mazungumzo ya busara kwa niaba yake.

Mtazamo huo huo unachukuliwa na Ahoua Don Mello, ambaye anagombea kama mgombea binafsi: alivuliwa wadhifa wake ndani ya Chama cha African Peoples' Party - Côte d'Ivoire (PPA-CI), chama cha Laurent Gbagbo. Ahoua Don Mello anaongoza mkutano huko Cocody, kisha ataendelea na mkutano huko Bouaké (katikati). Hana uuungwaji mkono rasmi kutoka kwa PPA-CI. Mgombea huyu anatetea wazo la uhuru wa kiuchumi kwa nchi. Mawazo atakayowasilisha "katika miji mikubwa na katika maeneo yenye makazi madogo," anasema.

Mke wa rais wa zamani Simone Ehivet atakuwa Bouaflé, katika eneo la kati. Ananuia kukutana na wazalishaji wa kakao wanaoishi huko. Hii ni njia ya kuangazia kipengele kimoja cha jukwaa lake: anaangazia usindikaji wa bidhaa za ndani.

Mwanamke mwingine katika uchaguzi huu, Henriette Lagou, pia atakuwa katika eneo la kati: atafanya mkutano wake tarehe 13 Oktoba huko Daaukro, ngome ya PDCI. Kauli mbiu yake: amani na mshikamano wa kijamii.

Hatimaye, mkuu wa nchi anayemaliza muda wake, Alassane Ouattara, atafanya mkutano wake siku ya Jumamosi tarehe 11 Oktoba huko Daloa, jiji lililo katikati-magharibi mwa nchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii