Watu 95 wafariki kutokana na njaa pamoja na magonjwa Sudan

Watu 95 wamekufa kutokana na njaa pamoja na magonjwa katika kipindi cha siku 40 zilizopita kwenye kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk huko El Fasher nchini Sudan, wafanyakazi wa kujitolea wamethibitisha.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na mashirika ya misaada ya kibinadamu, matukio hayo yanaonesha  hali inavyoendelea kuwa mbaya katika Mji wa El Fasher.

Kambi hiyo ambayo ilikuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi wa ndani zaidi ya Elfu 19 imekuwa ikishambuliwa na makombora na ndege zisizokuwa na rubani, vifo vya raia vikiripotiwa wakati maelfu ya wengine wakitoroka kutafuta mahali salama.

Mwishoni mwezi Agosti, wapiganaji wa RSF walishambulia kambi hiyo na kutekeleza mauaji ya karibia watu 40 na kuwateka wengine kulingana ripoti za wanaharakati wa haki za binadamu.

Haya yanaripotiwa wakati wito umetolewa kwa jamii ya kimataifa kushinikiza pande hasimu kwenye mzozo wa Sudan kuhakikisha raia wanalindwa haswa wanapotorokea kwenye maeneo salama.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii