Wanawake wanazidi kunyanyaswa kwenye mitandao

Kadri matumizi ya mitandao yanavyoongezeka barani Afrika, wanawake na wasichana wanazidi kuripoti ukatili kutokana na matumizi hayo ya mitandao.

Kwenye ripoti iliyotolewa na Shirikisho la Mawakili Wanawake nchini Kenya kwa ushirikiano (FIDA) na taasisi inayopigania haki za wanawake nchini Nigeria (WARDC), imebainika kuwa wanawake wanashuhudia ukatili wa hali ya juu katika shughuli zao za kila siku wanapotumia mitandao. Ripoti hiyo ikiashiria kuwa karibu kila mwanamke aliyehojiwa tayari amekumbana na aina fulani ya unyanyasaji mtandaoni – iwe ni udhalilishaji, ufuatiliaji (cyberstalking), au uchapishwaji wa picha za siri bila idhini.

Katika matokeo makuu ya utafiti huu, takwimu zinaonyesha hali ya kutisha. Kenya inarekodi zaidi ya 99% ya wanawake waliosema wamewahi kushuhudia ukatili kwenye mitandao, huku 97% wakikumbana na unyanyasaji wa kisaikolojia na 74% wakiripoti unyanyasaji wa kijinsia.

Nigeria nayo inatoa taswira yenye kufanana, ambapo zaidi ya robo tatu ya washiriki walieleza kunyanyaswa kupitia ujumbe wa matusi, picha za uchi zilizochapishwa bila ruhusa, na mashambulizi ya moja kwa moja kwenye majukwaa kama WhatsApp na Facebook. Vijana wa umri wa miaka 18–34, pamoja na wanaharakati, wanasiasa na wanahabari, ndiyo walijitokeza kuwa katika hatari kubwa zaidi.

Athari za ukatili mtandaoni zinaenea zaidi katika simu na tarakilishi. Waathirika wengi wanapata msongo wa mawazo, hofu na hata mawazo ya kujiua. Wengine hulazimika kufuta akaunti zao za mitandao ya kijamii na kuacha kuchangia kwenye mitandao, jambo linalosababisha upweke na kujitenga na jamii. Kuna pia madhara ya moja kwa moja kiuchumi na kielimu, ambapo baadhi hupoteza ajira, wateja, au nafasi za masomo kutokana na kampeni za udhalilishaji. Aidha, ukatili wa kidijitali mara nyingine huingia kwenye maisha halisi kwa namna ya kuviziwa na kupata vitisho.

Utafiti unaonyesha pia ni nani wanaoendesha mashambulizi haya. Nchini Nigeria, asilimia 86 ya wanyanyasaji walibainika kuwa ni watu wasiojulikana wanaotumia akaunti ghushi, huku Kenya ikirekodi takriban 46% ya mashambulizi kutoka kwa watu wasiofahamika. Aidha, wapenzi wa zamani wametajwa kuwa sehemu kubwa ya wanyanyasaji, wakitumia picha na video za uchi kwa kulipiza visasi. Hali hii inaonyesha jinsi ukatili wa karibu na ule wa siri mtandaoni unavyoshirikiana kuendeleza madhila dhidi ya wanawake.

CHANGAMOTO

Changamoto kisheria na kijamii zinabaki kuwa kikwazo kikuu katika mapambano dhidi ya ukatili huu. Nchi zote mbili zina sheria za kudhibiti uhalifu mtandaoni, lakini bado hazina mtazamo wa kijinsia. Polisi na mahakama mara nyingi hukosa utaalamu wa kushughulikia ushahidi wa kidijitali, huku unyanyapaa wa kijamii na ucheleweshaji wa haki vikizidisha tatizo. Kampuni za teknolojia pia zinakosolewa kwa ukosefu wa uwajibikaji, kwani mara nyingi ripoti za unyanyasaji huchukuliwa kwa urahisi au hupuuzwa.

MAPENDEKEZO

Mapendekezo ya hatua za haraka ni pamoja na kurekebisha sheria ili zitambue wazi ukatili wa kidijitali wa kijinsia, kuwekeza kwenye elimu ya usalama wa mitandao kwa wanawake na wasichana, na kujenga mifumo ya msaada wa kisaikolojia, kisheria na kijamii. Pia, mashirika ya teknolojia yanapaswa kuwajibishwa zaidi kwa usalama wa watumiaji wao, huku ushirikiano wa kikanda kati ya serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ukihitajika ili kuunda mkakati thabiti wa kupambana na ukatili huu.

Mwisho wa yote, ripoti hii inaweka wazi kwamba teknolojia si tatizo bali ni kioo kinachotoa taswira ya ukosefu wa usawa wa kijamii uliopo. Bila hatua thabiti, ukatili kwenye mitandao utaendelea kunyima wanawake na wasichana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa kidijitali. Lakini kupitia marekebisho ya sera, elimu, msaada wa kisaikolojia na uwajibikaji wa kampuni za teknolojia, bara la Afrika linaweza kugeuza mitandao kuwa chombo cha uhuru na siyo uwanja wa ukandamizaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii