Bibi adaiwa kuua mjukuu wake kisa kutomsalimia

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamsaka Christina Kishiwa (42), mkazi wa Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi, Manispaa ya Kahama, kwa tuhuma za kumuua mjukuu wake, Sofia Ndoni (4), baada ya kumshambulia kwa vipigo kisha kumkaba shingoni hadi kufariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea baada ya mtoto huyo kushindwa kumsalimia bibi yake asubuhi pamoja na kujisaidia kitandani. 

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtuhumiwa alicharuka na kuanza kumpiga mtoto huyo kwa fimbo na bomba la maji la plastiki sehemu mbalimbali za mwili wake kabla ya kumkaba shingoni.

"Mtuhumiwa alitoweka mara baada ya tukio hilo na juhudi za Jeshi la Polisi bado zinaendelea ili kuhakikisha anapatikana na kufikishwa mbele ya sheria," alisema Kamanda Magomi.

Aidha, Magomi alitoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuacha kutumia unyanyasaji kijinsia au vipigo kama mbinu ya malezi, kwani ni kinyume cha sheria na haki za watoto. 

Aliongeza kuwa ni muhimu watoto wakalelewa kwa maadili na heshima badala ya mateso.

Bakari Fundikira, mkazi wa eneo hilo, alisimulia kuwa alipita eneo la tukio akiwa anatoka harusini na kusikia mama mmoja akiomba msaada.

Alipofika, alikuta mama mzazi wa mtoto akiwa amembeba mwanawe aliyekuwa tayari amelegea. 

Baadaye, mama mdogo wa marehemu alifika na kubaini kuwa mtoto alikuwa amefariki dunia huku akiwa na majeraha ya vipigo mwilini.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakato, Hussein Mwita, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa alijaribu kuficha ushahidi kwa kuusafirisha mwili kimya kimya kwenda kuuzika kijijini kwao bila kuujulisha uongozi wa mtaa. 

Alidai kuwa Kishiwa ana historia ya matukio ya ukatili, na kwamba tayari alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kumdhulumu msichana wa kazi.

"Mama huyu si mara ya kwanza kutuhumiwa kwa ukatili. Tulikuwa na kumbukumbu zake na hata kesi yake ipo polisi," alidai Mwenyekiti Mwita.

RIPOTI YA DAKTARI

Dk. Michael Mushi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, alisema walipokea mwili wa mtoto huyo usiku wa kuamkia Septemba 29, ukiwa na majeraha ya wazi sehemu mbalimbali za mwili.

"Uchunguzi umebaini kuwa mtoto alipigwa kwa kitu kizito chenye umbo bapa. Alikuwa na majeraha kichwani, mgongoni, kifuani, mikononi na tumboni – na yote haya yalisababisha kifo chake," alisema Dk. Mushi.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku likitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za aliko mtuhumiwa Christina Kishiwa kuwasiliana na kituo cha polisi kilicho karibu au kupiga namba za dharura ili kuhakikisha haki ya mtoto inapatikana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii