Mgombea urais AAFP kumaliza kero Soko la Songea ndani ya siku 90

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, ameahidi kumaliza kero za soko kuu la mkoa wa Ruvuma ndani ya siku 90 endapo atachaguliwa kuongoza nchi.

Akihitimisha kampeni zake mkoani Ruvuma kwa kutembelea soko kuu la Songea jana, Mwiru alisema hayuko tayari kuona wafanyabiashara wakiendelea kufanya shughuli zao katika mazingira yasiyo rafiki.

“Mkinichagua, ndani ya siku 90 nitazenge soko lote. Haiwezekani saraji ipo, halafu baadhi ya wafanyabiashara wanafanyia shughuli zao chini ya vumbi,” alisema.

Mbali na suala la soko, mgombea huyo aliahidi kushughulikia changamoto zote zinazowakabili wakulima, ikiwamo uhaba wa mbolea na ukosefu wa masoko ya uhakika ya mazao yao.

Mwiru, ambaye chama chake kimejikita katika masuala ya kilimo, aliwataka wananchi kumpa kura Oktoba 29 ili aweze kushirikiana nao kutatua matatizo yanayowakabili.

“Ninawahakikishia kuwa nitahakikisha wakulima na wafanyabiashara wa hapa sokoni mnakuwa huru kufanya kazi zenu na kunufaika na jasho lenu,” alisisitiza.

Ameongeza kuwa chama chake kitahakikisha anafika hadi mashambani kujionea hali halisi ya kilimo na kupata maoni ya moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Baada ya kumaliza kampeni zake mkoani Ruvuma, Mwiru anatarajiwa kuendelea na mikutano mkoani Njombe na kisha Mbeya, huku akiahidi hatua kali dhidi ya mafisadi, ikiwamo “kufuga mamba Ikulu watakaowatafuna wala rushwa.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii