Mgombea urais Salum Mwalimu aahidi uwekezaji mkubwa kupitia Kituo cha PPP

Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amemtumia salam Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, kujiandaa na "mapinduzi makubwa" ya uwekezaji kwenye kituo hicho, ambacho amepanga kukitumia kwa miradi mikubwa ya maendeleo endapo atapewa ridhaa ya kuingia Ikulu.

Mwalimu amesema kuwa, kama Watanzania watamchagua kuwaongoza kwenye uchaguzi mkuu ujao, yupo tayari kuwekeza fedha nyingi kwenye Kituo cha PPP ili kuendesha miradi itakayobadilisha uchumi wa nchi.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Muleba, mkoani Kagera, Mwalimu alisema:

“Tanzania tuna Kituo cha Uwekezaji na Mitaji ya Umma, na anayekiendesha ni rafiki yangu, David Kafulila. Ajiandae kwa sababu tutatumia kituo hiki katika mambo yote ya msingi ya taifa. Tutaweka fedha za kutosha ili kuwezesha huduma zote za kibinadamu na miradi itakayochechemua uchumi na kuongeza uzalishaji.”

Miongoni mwa miradi aliyoeleza Mwalimu kuwekeza ni pamoja na kuanzisha boti za mwendokasi katika Ziwa Victoria ili kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Aidha, Mwalimu ameahidi kwamba endapo atapewa mamlaka, atasitisha mipango yote ya serikali ya kupanua hifadhi au mapori ya hifadhi hadi atakapojiridhisha kuwa mahitaji ya binadamu yametosheleza.

“Kwenye miradi yote muhimu ya taifa, tutatumia Kituo hiki kuweka fedha za kutosha, kuhakikisha huduma zote za msingi zinapatikana na kuongeza uzalishaji wa taifa,” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii