Vilio zaidi kwa polisi, wawili wakidaiwa kufariki kwa kipigo Moro, Tabora

Madai ya watuhumiwa kufariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi au baada ya kipigo cha askari hao yameendelea kujitokeza safari hii yakiibuka katika mikoa ya Tabora na Morogoro.

Katika matukio hayo mawili, moja linamhusu mmoja wa vijana walituhumiwa kuiba msumeno wa umeme wa mbao, Koba Ndalu (23) wa Kilosa mkoani Morogoro na lingine la Jacob Elias mkazi wa Gongoni Manispaa ya Tabora.

Vifo hivyo vimetokea ikiwa ni takriban siku 10 tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipomwagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuunda kamati ya kuchunguza mauaji ya mfanyabiashara wa madini yaliyotokea Januari 5 mkoani Mtwara.

Vilevile, Rais Samia alitaka kamati hiyo ambayo iliundwa na waziri mkuu baadaye siku hiyohiyo ichinguze pia mauaji ya watu siya yaliyotokea wilayani Kilindi mkoani Tanga yakihusisha wakulima na wafugaji.

Tayari maofisa saba wa polisi wameshafikishwa mahakamani kutokana na mauaji hayo, huku mmoja wa maofisa waliohusishwa na tukio hilo akidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu mkoani humo.

Koba na mwenzake mwenzake walikamatwa Februari 2, mwaka huu lakini baadaye alitolewa akiwa hoi baada ya kudaiwa kupigwa na mauti yakamkuta Februari 7 katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa alikokuwa amelazwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim hakupatikana mara kadhaa kwenye simu yake iliyokuwa inaita mrefu bila kupokewa.

“Afande Fortunatus Musilimu yupo darasani anafundisha na hayupo kabisa Morogoro, yupo Zanzibar na anatarajia kurudi wiki ijayo,” alisema msaidizi wake kupitia simu yake.

Hata hivyo, Kaimu mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Abubakari Kunenge alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kuwa na taarifa nalo na kuwa mamlaka ya juu imetoa mwongozo wa kushughulikia matukio kama hayo.

“Kwa taarifa iliyopo na niliyopewa ni kwamba marehemu Koba Ndalu hajafia mahabusu bali amefia hospitali na mambo yenye mazingira kama haya tayari mamlaka (Rais Samia) imeyatolea mwongozo siku chache zilizopita,” alisema Kunenge.

“Hili litashughulikia kwa utaratibu huo huo na Serikali itatoa mrejesho kwa sababu mamlaka imetoa na kuna masuala yenye mazingira yenye changamoto na tuhuma kama hizi na Serikali italishughulikia katika mstari kama huohuo na hiyo ni taarifa ya mwanzo niliyopewa,” aliongeza.

Akizungumza na Mwananchi juzi hili, Machinda Omari (26) aliyekamatwa pamoja na Ndalu, alisema walifikishwa Kituo cha Polisi Kilosa wakituhumiwa kuvunja na kuiba msumeno wa umeme mali ya Dotto Machungwa mkazi wa Kichangani, Kilosa.

Machinda alisema walikanusha tuhuma hizo na kutakiwa kutoa maelezo na kisha kuwekwa mahabusu.

“Tulikamatwa Jumatano Februari 2, asubuhi na askari wa polisi jamii na sote tulikana tuhuma,” alisema Machinda.

Alisema ilipofika saa 11 jioni siku hiyo, alifika askari (anamtaja jina) na kufungua mlango wa mahabusu na kuuliza, “Machinda na Koba mpo?”

“Tuliitika na kutolewa huku tukielezwa na askari huyo kuwa tunaenda gereji, yaani chumba cha mateso.

“Nilivua nguo zote kwa maelekezo yake kisha kunifunga kamba kwenye magoti halafu katikati ya mapaja palipenyezwa mti na nilinyanyuliwa kisha kuning’inzwa juu kati ya meza moja na nyingine na kuanza kupigwa mwilini nikitakiwa kukubali kuwa nimeiba msumeno wa umeme,” alidai Machinda.

Baada ya kutoka yeye katika chumba cha mateso, alidai kuwa Koba Ndalu alifuatia kuteswa katika mfumo huohuo wakilazimishwa kukubali kuwa wametenda kosa hilo la wizi.

Alidai mateso hayo yalifanyika kwa siku mbili kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

“Kutokana na mateso hayo Koba hakuweza kula, kwenda chooni pekee yake wala kutembea na badala yake chakula alikuwa akilishwa, alikuwa akibebwa kwenda chooni kutokana na kupata maumivu makali kwenye maungio ya mwili wake, yakiwemo magoti,” alidai Machinda.

Machinda anadai alipata dhamana Februari 5 na alipofika kwa ndugu zake aliwaeleza kuwa mwenzake Koba hawezi kula, kwenda chooni wala kutembea na amekuwa mtu wa kulishwa chakula na kunyanyuliwa na mahabusu wenzake kwa kusaidiwa kila jambo kama mlemavu wa viungo.

Naye Kenneth Sajilo, jirani wa marehemu Koba alisema baada ya kupata taarifa hizo walifuatilia kwa ukaribu zaidi wakati wa kupeleka chai na chakula lakini hawakuweza kumuona katika mahabusu hiyo.

“Nilienda Jumapili (Februari 6) kupeleka chakula sikuweza kumuona Koba na saa 10 jioni nilipata taarifa ya uwepo wa mahabusu kuwa yupo hospitali ya Wilaya Kilosa wodi namba 6 na nilienda kumuona jioni nikakuta akiwa katika hali ya maumivu,” alisema Sajilo.

Sajilo alidai, Koba alikuwa chini ya ulinzi wa askari polisi hapo wodini na alifanikiwa kumjulia hali kwa kumdadisi juu ya tukio lao la kutuhumiwa kuiba msumeno wa umeme na kumuuliza kwa nini amelazwa katika hospitali hiyo.

Sajilo alisema wale askari walimweleza kuwa huyo ‘ndugu yako Koba Ndalu amelazwa hapo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari’.

“Nilipoongea naye jioni ile, kabla ya umauti kumfika akiwa hospitali, Koba aliniambia anaumwa sana na amepigwa sana,” alidai Sajilo akimnukuu Koba Ndalu.

Sajilo alidai kuwa yeye alimwambia Koba kuwa ni jambo la kawaida kwa binadamu kukamatwa na kutuhumiwa huku mtuhumiwa huyo akidai kumueleza kuwa endapo angeiba msumeno na kipigo alichopigwa isingekuwa rahisi kuendelea kupata mateso bali angeonyesha ulipo lakini hajatenda kosa hilo,” alidai Sajilo.

“Ilipofika asubuhi ya Jumatatu ya Februari 7, nilipata taarifa za kifo cha Koba kuwa amefariki dunia,” alisema Sajilo.

Binamu wa marehemu, Chilongola Robert (33) alisema wamepata ripoti ya daktari wa hospitali hiyo iliyoonyesha kuwa ndugu yao amefariki baada ya kupata kipigo.

Alisema ripoti hiyo imekabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Alhaji Majid Mwanga ambaye aliwaeleza ndugu waliokwenda ofisi kwake.

“Askari waliokuwa wakimlinda pale haspitali waliondoka baada ya Koba kufariki dunia na baada ya uchunguzi wa kifo chake kuonyesha kimetokana na kipigo kwa sababu mkuu wa wilaya ametueleza katika kikao cha ndugu, kufuatia sisi kuwa na mashaka na kifo cha ndugu yetu,” alidai Chilongola.

Alisema katika kikao hicho na mkuu wa milaya walikubaliana kuwa Serikali igharamie mazishi ambayo tayari yamefanyika mkoani Dodoma.

DC Mwanga alipoulizwa kuhusu tukio hilo alijibu kwa ufupi kuwa Serikali ya wilaya inatambua uwepo wa tukio hilo na wanalishughulikia.

Mwanga alisema ni sahihi tukio hilo limetokea na uongozi wa wilaya na vyombo vyake vya ulinzi na usalama wanalifuatilia ili kupata ukweli wa jambo hilo na akaomba wamepewe muda kidogo wa kufuatilia.

Ilivyokuwa Tabora

Hali ikiwa hivyo Kilosa, mkoani Tabora nako Jeshi la Polisi limeingia kwenye tuhuma za kusababisha kifo cha mahabusu aliyekuwa anashikiliwa kwa tuhuma za wizi wa nguo na fedha Sh45,000.

Mtuhumiwa huyo, Jacob Elias mkazi wa Milanzi Kata ya Gongoni, Manispaa ya Tabora alifariki dunia juzi jioni ikidaiwa kifo chake kimesababishwa na kipigo alichokipata kutoka polisi alipokuwa akishikiliwa mahabusu.

Akizungumza na Jembe FM, baba mdogo wa marehemu, John Mashishanga alidai mtoto wake alifariki dunia muda mfupi baada ya kuachiwa kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Tabora alikokuwa akishikiliwa.

Mashishanga alidai alipata taarifa za kifo cha mtoto wake ambaye alipelekwa nyumbani kwa Bajaj na mtu aliyedai kuwa amemsaidia kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.

“Nilienda kuuona mwili wa marehemu nyumbani kwa dada yangu na kuukuta ukiwa na majeraha kwenye sehemu mbalimbali kama mgongoni na miguuni,” alidai Mashishanga.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao ili azungumzie tukio hilo, akasema bado hajapata taarifa za tukio hilo lakini akaahidi kulifuatilia kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tabora (OCD) kisha angetoa taarifa.

Hata hivyo, alisema kama kuna madai hayo kwa sasa si rahisi kusema kwa sababu inawezekana chanzo cha kifo chake kikawa kingine na si kama wanavyohisi wanandugu.

“Uchunguzi wa chanzo cha kifo ukifanyika mdipo itajulikana sababu ya kifo na si vinginevyo,” alisema Kamanda Abwao.

Akisimulia zaidi kuhusu tukio hilo, Mashishanga alidai kuwa alielezwa kuwa Elias alifikishwa nyumbani akiwa hajiwezi na dada zake walimpokea na kumsaidia kumwingiza ndani.

“Lakini hakuchukua dakika akafariki dunia, tukachukua mwili na kuupeleka kuuhifadhi hospitali, lakini tulimweleza mwenyekiti wa mtaa ambaye alifika nyumbani na tukashaurina na wanandugu twende polisi tukaulize nini kimempata huyu bwana, kwa sababu alikuwa na walituambia ili kumtoa ni lazima tukamwekee dhamana. Imekuwaje ameachiwa tena akiwa amepigwa vibaya,” alidai Mashishanga.

Hivyo, alisema kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Mtaa, Kabi Omary waliamua kumtuma (Mashishanga) aende polisi kufuatilia zaidi.

“(Jumamosi) Nilienda Polisi, nilipofika pale nikamkuta askari wa kike pale mapokezi nikamweleza kuwa nimeenda kumwekea dhamana Jacob Elias.”

“Kwa sababu mahabusu iko jirani tu hapo, yule askari akaita jina la Jacob, lakini mahabusu wengine wakajibu ametoka jana yake yaani Ijumaa.

Mashashangaa anadai kuwa alimuuliza yule askari ndugu yao amedhaminiwa na nani, lakini “hakutaka kutujibu ila akaniambia muda ule alikuwa na kazi nyigi, kwa hiyo turudi Jumatatu tukachukua RB namba na jina la mpelelezi,” alieleza.

Dada wa marehemu, Monica Elias, alisema siku hiyo akiwa ndani na ndugu yake, Anastazia, kuna mtu alifika na kubisha hodi wakamkaribisha akajitambulisha ni dereva wa Bajaj.

Akawaeleza kuna mzee amemleta kwa hiyo watoke wakamchukue kama wanamfahamu.

“Tulitoka, tulipofika kwenye Bajaj tukamtambua ni Jacob, lakini alikuwa ameumia sana, hawezi hata kujisogeza na alikuwa anazungumza kwa shida, tukambeba na kumwingiza ndani tukisaidiwa na yule aliyemleta,” alidai Monica.

“Tulipomuuliza alikomtoa ndugu yetu, alidai kamsaidia kutoka hospitali ya Kitete na yeye ndiye aliyemwelekeza hapa nyumbani,” alidai Anastazia.

Alidai walipomuuliza Jacob nini kimempata, aliwaeleza kwa shida kuwa amepigwa na polisi akiwa mahabusu na ana maumivu makali.

Jacob alikuwa akifanya kazi ya ulinzi eneo la Kanyenye katika grosari moja ambayo hata hivyo hawakuitaja jina.

Akisimulia mkasa huo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Milanzi, Omary alisema alipewa taarifa na ndugu wa marehemu kuwa ndugu yao kapigwa na Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma ya wizi.

“Tayari tumewasiliana na mamlaka husika kwa hatua zaidi kwa sababu suala liko nje ya uwezo wake,” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii