KESI ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeendelea kuwa moto mahakamani, safari hii akigoma kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, akilalamikia kile alichokiita "kuondolewa kwa wafuasi wa chama kwa amri ya maofisa wa polisi".
Tukio hilo lilijiri jana majira ya saa 3:29 asubuhi, Lissu alipowasili mahakamani akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Jeshi la Magereza na kuingia katika chumba cha wazi namba moja. Alipowasili, Lissu alinyanyua mkono wake na kuuzungusha juu ya kichwa, akipokewa kwa ishara hiyo hiyo, lakini kwa ukimya kutoka kwa wafuasi waliokuwa ndani ya ukumbi huo.
Muda mfupi baadaye, jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde liliingia mahakamani.
Wafuasi waliokuwamo ndani, wakiwamo viongozi wa juu wa CHADEMA walioongozwa na Godbless Lema, walianza kutoka ukumbini kimyakimya kwa ishara za mikono, hali iliyozua sintofahamu na kusababisha kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi.
Wengine walidai kuwa walizuiwa kuingia ukumbini kwa maelekezo ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO), jambo lililosababisha Lissu kuwasilisha pingamizi, akitaka mahakama iwarejeshe watu hao ukumbini kabla ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
"Hii siyo mahakama ya kijeshi bali ya kiraia. Ni majaji pekee wenye mamlaka ndani ya ukumbi huu, siyo polisi wala maofisa wa upelelezi," alisisitiza Lissu.
Alidai kuwa kesi hiyo ni ya aina ya kipekee – ya uhaini – na hivyo ni lazima ifanyike kwa uwazi na kuheshimiwa kwa viwango vya juu vya haki.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, alipinga hoja hiyo akisema kuwa hakuna ushahidi wa kuondolewa kwa watu hao kwa amri ya polisi, na kwamba mahakama haiwezi kuahirisha usikilizwaji kwa msingi wa watu kutokuwapo.
"Mahakama hii ni ya wazi, lakini pia inaruhusu idadi ya watu kulingana na uwezo wa ukumbi. Hakuna ushahidi wa amri kutoka kwa ZDCO, watu waliondoka kwa hiari yao," alidai Wakili Katuga.
Jaji Ndunguru, akitoa uamuzi wa awali, alieleza kuwa mahakama haikupokea taarifa yoyote rasmi inayothibitisha kuwapo amri ya polisi ya kuondoa watu ukumbini, na alisisitiza kuwa utulivu uendelee.
Jaji Ndunguru pia alisema waliona namna ya watu walivyokuwa wanahamasishana kutoka kwa kutumia ishara za mikono.
"Kama ingekuwapo amri hapa tungeiona. Huu ni ukumbi wa wazi, hauwezi kuchukua watu wengi, ule utaratibu uliotumika wiki ukiyopita uweze kuendelea kwa sababu hakukutokea jambo lolote ni utaratibu mzuri.
"Nitoe maelekezo kama kuna tatizo limetokea tuwe wavumilivu, wale waliyokuwapo wangeendelea kubaki. Mahakama inaelekeza kama kuna jambo lolote limetokea lipatiwe ufumbuzi kabla hatujaingia mahakamani," alisema Jaji Ndunguru
Dakika chache baadaye, baadhi ya wafuasi waliokuwa wameondoka walirejea mahakamani, na mwenendo wa kesi uliendelea.
Katika hatua iliyofuata, Lissu aliwasilisha mapingamizi kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka pamoja na vielelezo vya upande wa mashtaka, hasa maelezo ya mashahidi ambao ni askari polisi.
"Maelezo ya mashahidi 23 kati ya 30 ni batili kwa mujibu wa sheria, yameandikwa na kutiwa saini na mtu mmoja bila kuzingatia taratibu za kisheria.
"Pia, taarifa zao zinaeleza majina, makazi, ajira na hata namba za simu – tofauti kabisa na amri ya mahakama ya kulinda usiri wa mashahidi," alidai Lissu.
Pia alilalamikia mabadiliko kwenye hati ya mashtaka yaliyofanywa bila rukhsa ya mahakama, akisisitiza kuwa hati hiyo haioneshi kosa linalomkabili, na hivyo kesi hiyo inapaswa kufutwa.
"Nimeshikiliwa kwa siku 162 kwa hati isiyo halali. Ninaomba mahakama itumie mamlaka yake kufuta kesi hii," alisema Lissu kwa msisitizo.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Wakili Katuga aliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18 mwaka huu ili upande wa Jamhuri upate muda wa kujiandaa kujibu hoja zilizotolewa na mshtakiwa. Mahakama iliridhia ombi hilo.