Nchini Uganda, sasa inajulikana Yoweri Museveni atapambana na nani katika uchaguzi wa urais wa mwezi Januari 2026. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, Septemba 24, Tume ya Uchaguzi imetangaza kwamba wagombea wanane kati ya 38 wamepasishwa. Miongoni mwao ni rais wa sasa, aliye madarakani tangu mwaka 1986, na mpinzani wake mkuu, mwinamuziki wa zamani Bobi Wine. Kuidhinishwa kwa kugombea kwake hakukuwa na uhakika hadi dakika ya mwisho.
Nchini Uganda, kuanza kwa kinyang'anyiro cha urais tayari kunazua hasira miongoni mwa wanasiasa, na mchakato huo umegubikwa na ukosoaji. "Umeingia kama mgombea anayesita sita, unajikuta kuwa mgombea rasmi." Amesema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Simon Mugenyi Byabakama, alipokuwa akipitisha wagombea wanane kuwania kwenye kinyang'anyiro cha urais mwakani.
Saa chache kabla ya kuanza kwa mchakato huo, Tume ya Uchaguzi imewatahadharisha baadhi ya wagombea kuwa hawakuwa na idadi inayohitajika ya saini za kugombea. Siku ya Jumanne asubuhi, takriban wagombea ishirini waliokatishwa tamaa waliomba kuahirishwa kwa uamuzi huo, wakisema kwamba waliarifiwa wamechelewa mno.
Yoweri Museveni, anajulikana kuwa ni mgombea asiyepingika. Akiwa na umri wa miaka 81, anawania muhula wa saba wa miaka mitano baada ya kufanya marekebisho ya Katiba na kuondoa ukomo wa mihula. Kwa hiyo Museveni anaungana na wagombea wengine kama vile Frank Bulia Kabinga, Robert Kasibante, Joseph Mabirizi, Nandala Mafabi, Grégory Mugisha Muntu, na Mubarak Munyagwa, ambao walipishana kwa zamu kwa siku mbili chini ya hema kubwa la Tume ya Uchaguzi.
Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, ambaye alifika katika Tume ya Uchaguzi katika wingu la vumbi lililorushwa na pikipiki za kukodiwa zilizomzunguka, pia yuko kwenye orodha ya mwisho. Akiwa mpinzani mkali, alikamatwa mara nyingi na amekuwa akilengwa na mashambulizi makali ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais. Mnamo mwaka 2021, alimaliza wa pili katika duru ya kwanza ya uchaguzi, akipata 34.8% ya kura. Katika hotuba yake aliyoitoa dakika chache baada ya kuidhinishwa kwake kuthibitishwa, kiongozi huyo wa upinzani alitoa wito kwa wafuasi wake kumuunga mkono "kwa utulivu na nidhamu."
Huku wagombea wakiwa tayari, kampeni zimepangwa kuanza Septemba 29.