Nchini Malawi, Chama tawala cha Rais Lazarus Chakwera kinadai kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita huku chama hicho kikidai kuwa na ushaihidi wa kutosha wa kudhibitisha hilo.
Kulingana na matoeko ya awaili ya uchaguzi uliofanyika tarehe 16 mwezi huu, Chama cha Malawi Congress Party MCP kimeonekana kuzoa idadi ndogo ya kura kutoka kwa baadhi ya wilaya ambazo tayari hesabu zimekamilika.
Mgombea mwenza wa MCP Vitumbiko Mumba amesema kuwa wana ushahidi kwamba baadhi ya watu walikuwa wanajaza karatasi za kupigia kura kwenye masanduku ya kupigia kura huku akisema kuwa matokeo ya awali hayalingani na takwimu zilizotangazwa katika kituo cha kujumlisha kura.
Aidha MCP imewasilisha malalamiko kwa Tume ya Uchaguzi ya Malawi wakati ambapo Chama cha Democratic Progressive Party DPP kilikariri kuwa hesabu zake zilionyesha kuwa mgombea wake wa urais Peter Mutharika anaongoza kura hizo kwa sasa.
Baada ya MCP kudai Ijumaa kuwa kulikuwa na dosari katika upigaji kura, polisi walitangaza kukamatwa kwa wafanyikazi wanane wa kuingiza data.
Rais Lazarus Chakwera aliingia madarakani katika marudio ya uchaguzi 2020 baada ya uchaguzi wa 2019 kufutwa kwa sababu ya udanganyifu.
Tume ya uchaguzi nchini humo ina hadi Jumatano kutoa matokeo ya mwisho ya kura ya urais.