Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama
ameipongeza Mamlaka ya Serikali Matandao (eGA) kwa kutengeneza mfumo
utakaowezesha mifumo mbalimbali ya Serikali kubadilishana taarifa, jambo
hili ni hatua kubwa katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya
TEHAMA ndani ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa wakati
wowote.
Akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo jijini Dodoma,
Waziri Mhagama amefurahishwa na utekelezaji wa haraka wa agizo hilo na
kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha mifumo yote ya
TEHAMA inayotumiwa ndani ya Serikali inawasiliana na kubadilishana
taarifa ili kurahisisha utoaji huduma kwa umma.
“Ninatoa pongezi
nyingi kwa Mamlaka kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais kwa wakati na
ninafahamu kuna baadhi ya taasisi za umma zimeshaunganishwa katika mfumo
huo, hivyo ninaagiza kazi ya kuunganisha taasisi zilizobaki ikamilike
kwa wakati na kufanya kazi kama ilivyodhamiriwa” Alisema Mhe.Mhagama.
Aidha,
Mhe. Mhagama ametoa wito kwa watanzania kuendelea kutumia mifumo ya
TEHAMA iliyobuniwa, kusanifiwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani
katika shughuli zao za kila siku kwani zinarahisisha sana utendaji kazi,
kupunguza gharama na mianya ya rushwa.
Pia, Mhe. Mhagama
amesisitiza na kuwataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa
kufuata maadili ya Utumishi wa Umma hasa wanapotumia mifumo ya
kidijitali kwa uzalendo na uwajibikaji ili kumsaidia Mhe. Rais katika
kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi kama kaulimbiu ya awamu ya sita
ya “Kazi Iendelee” inavyosadifu.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji
wa Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama,
Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Benny Ndomba amesema katika
utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais, Mamlaka imetengeneza mifumo
mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini
(MUTAS) ambao mpaka sasa umeunganisha na unatumiwa na taasisi kumi kwa
hatua ya majaribio.
Katika taarifa yake, Mhandisi Ndomba
ameainisha baadhi ya mifumo mingine iliyotengenezwa na eGA kwa
kushirikiana na taasisi husika na kwa kutumia wataalamu wa ndani kuwa ni
Mfumo wa Ukusanyaji Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG) unaosimamiwa
na Wizara ya Fedha na Mipango, Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Ankara kwa
Mamlaka za Maji nchini (MAJIIS) unaosimamiwa na Wizara ya Maji, Mfumo wa
Kusimamia Rasilimaliwatu Serikalini (New HCMIS) unaosimamiwa na Ofisi
ya Rais Utumishi, Mfumo wa kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi
(ERMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) na Mfumo wa Baruapepe
Serikalini (GMS).
Ziara hiyo ya Waziri Mhagama kwenye Ofisi ya
Mamalaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma iliyofanyika Februari 11,
2022 ni sehemu ya kuzitambua taasisi zote zilizopo chini ya Wizara yake
ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.