Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameomba radhi kufuatia shambulizi lililofanywa na vikosi vya ulinzi vya nchi yake katika Hospitali ya Al-Nasser, Ukanda wa Gaza, lililoua watu wasiopungua 20 wakiwemo waandishi wa habari watano. Akizungumzia tukio hilo, Netanyahu amelieleza kama “msiba mzito” na kusisitiza kwamba Israel inatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari pamoja na raia wengine.
Hata hivyo, upande wa Palestina umeeleza kuwa radhi za Netanyahu hazitoshi, ukisema kitendo hicho ni “uendelezaji wa jinai dhidi ya ubinadamu.” Viongozi wa Palestina wametaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti badala ya maneno ya pole.
Mashirika ya kimataifa yakiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la Haki za Binadamu (HRW) na Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) yamelaani shambulizi hilo, yakisisitiza kuwa hospitali na wanahabari wanalindwa chini ya sheria za kimataifa za kivita. Mashirika haya yameitaka Israel kufanya uchunguzi huru na kuhakikisha uwajibikaji.
Wakati huo huo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa matukio kama haya yanazidisha hali ya taharuki na kuondoa matumaini ya upatikanaji wa amani ya kudumu katika Ukanda wa Gaza, huku raia wakiendelea kubeba gharama kubwa ya vita.