Wakati ugonjwa wa Chikungunya ukisambaa kwa kasi nchini China na kuambukiza zaidi ya watu 7,000 mamlaka zimeibuka na mbinu ya kuachia mbu wakubwa wasio na uwezo wa kung’ata binadamu ili kula mabuu ya mbu wanaoeneza virusi hivyo.
Mbu hao, wanaoitwa kitaalamu Toxorhynchites na kufahamika kwa jina maarufu la “mbu tembo”, hutumia mabuu ya mbu wadogo aina ya Aedes aegypti kama chakula. Wataalamu wanasema hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya mbu waenezao ugonjwa huo hasa katika mji wa Foshan mkoani Guangdong, ambako ndiko kitovu cha maambukizi.
Aidha Serikali imeanzisha operesheni maalumu ya kudhibiti ugonjwa huo kwa kutumia teknolojia na mbinu mbalimbali ikiwamo kurusha droni kutambua mazalia ya mbu, kutoza faini kwa wananchi wanaoacha maji kutuama, pamoja na kuachia “mbu tembo” ambao mabuu yake hula mabuu ya mbu wa Aedes, wanaosababisha Chikungunya.
Pia Serikali inatoa wito kwa wananchi kuondoa mazalia ya mbu majumbani na kutumia njia za kujikinga ikiwamo kuvaa nguo zinazofunika mwili, kutumia viuadudu na kuhakikisha madirisha na milango ina nyavu.
Shirika la Kudhibiti Magonjwa (CDC) la Marekani limetoa tahadhari ya kusafiri (Level 2) kwa watu wanaoelekea Guangdong, likiwashauri kuchukua tahadhari zaidi na kupata chanjo kwa wanaostahili.