Israel yafanya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa WHO

Jeshi la Israel limevamia maghala na majengo mengine ya Shirika la Afya Duniani, WHO, katika Ukanda wa Gaza wakati ikiendesha operesheni zake.

Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kwenye taarifa yake kwamba makaazi ya wafanyakazi wa shirika hilo katika mji wa Deir al Balah katikati ya Ukanda wa Gaza yalishambuliwa  mara tatu pamoja na ghala lake kuu la kuhifadhi dawa.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba jeshi la Israel lilivamia majengo hayo ya WHO na kuwalazimisha wanawake na watoto kuondoka na kuelekea Al Mawasi kwa miguu wakati vita vikiendelea.

Wafanyakazi wa kiume waliteswa kwa kufungwa mikono, kuvuliwa nguo na kuhojiwa huku wakishikiwa bunduki. Wafanyakazi wawili na watu wawili wa familia  zao walikamatwa. WHO imelitolea mwito jeshi la Israel kuwaachia huru mara moja wafanyakazi wake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii