Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dkt Dorothy Gwajima ameleleza kufanikiwa kusambaratisha ndoa ya mtoto wa Darasa la Sita iliyokuwa imefungwa katika kata ya Mbarali Zenga Mkoani Tabora.
Kupitia taarifa aliyochapisha katika mtandao wake wa Instagram Gwajima amewapongeza wananchi kwa kumpa ushirikiano wa kusambaratisha ndao hiyo ya mtoto wa Darasa la Sita aliyekuwa ameozeshwa kwa lazima na wazazi wake.
"KISA; Tarehe 6 Julai, 2025 Jumapili, jioni majira ya saa 9 nilipokea taarifa ya ujumbe wa simu (sms) kutoka kwa mwananchi mzalendo kutoka huko Tabora, Nzega, kuwa: kuna mwanafunzi wa darasa la 6 kaozeshwa kwa nguvu na wazazi wake na kuna juhudi za kuficha hizi taarifa. Aidha, mwananchi alisema, wanaofanyiwa hivyo wakikataa wanafukuzwa makwao.
HATUA NILIZOCHUKUA; kuwapa taarifa mamlaka ya mkoa husika ili Sheria ya mtoto ifanye kazi yake.
MATOKEO; Mwananchi mzalendo mtoa taarifa amenitumia ujumbe kuipongeza Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, tayari mtoto aliyeolewa ametafutwa na amepatikana kutoka huko alikofichwa pia, waliohusika wametiwa nguvuni kwa maelezo na hatua zaidi. Taarifa zaidi zitatolewa na mamlaka husika.
FUNZO; Ndugu Wananchi, mawasiliano ya kidigitali ni msaada mkubwa kwenye ulimwengu wa leo katika kuelimisha umma, kupokea na kupeleka taarifa na kuchukua hatua kwa gharama nafuu kabisa hivyo, tuendelee kushirikiana zaidi kupitia hii fursa kwani, tunafikika hadi vijijini.
HITIMISHO; Binti atarejea shuleni na waliohusika watapambana na sheria. Aidha, Nakemea Waoaji na Waozaji wa Watoto/ Wanafunzi. Nawataka jamii iache kuoa na kuoza Wanafunzi maana, utaratibu huo umepitwa na wakati. Hivi sasa, wananchi wako macho na taarifa zinasafiri kwa kasi.
MIKAKATI ZAIDI; Tutawafikia waharibifu wa watoto popote walipo. Wote mliowaoa wanafunzi, warejesheni shuleni mara moja kabla hatujawafikia. Timu yangu na mimi binafsi, tutaendelea kupokea sms za wananchi kuhusu masuala ya wizara hii na kuchukua hatua na kutoa mrejesho ili, kuwatia moyo zaidi wananchi.