Syria yalengwa na mashambulizi usiku, Israeli yaongeza maonyo

Syria imelengwa na mashambulizi mapya ya Israeli wakati wa usiku wa Julai 15 kuamkia Julai 16, hasa dhidi ya miundombinu ya kijeshi. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amefafanua nia ya Israeli. Shirika la Haki za Kibinadamu la Syria limeripoti vifo 248 tangu Julai 13 na kushutumu vikosi vya serikali ya Syria kwa kuwaua raia zaidi ya ishirini kutoka jamii ya Druze tangu kutumwa kwao katika mji wa Sweida.


"Lengo letu," ametangaza Benjamin Netanyahu, "ni kudumisha eneo la kusini magharibi mwa Syria kama eneo lisilo na wanajeshi. Hatutaruhusu," ameongeza, "kuanzishwa kwa Lebanon ya pili katika eneo hili." Na Jumatano hii asubuhi, Waziri wa Ulinzi wa Israeli Israel Katz, kwa upande wake, ametoa wito kwa Syria "kuwaacha kwa usalama Wadruze huko Sweida." "Kama tulivyoeleza kwa uwazi na kuonya, Israeli haitawaacha Druze nchini Syria na itatekeleza sera ya kuwaondoa wanajeshi ambao tumeamua," amesema katika taarifa yake. Vikosi vya Syria vinapaswa kuondoka, ameongeza, na ameahidi kudumisha mashambulizi ya kijeshi ya Israeli hadi hili lifanyike, akisema kwamba Israeli "itaongeza kiwango cha majibu dhidi ya utawala kama ujumbe hautaeleweka."

Jeshi la Israel limedai kushambulia kwa bomu lango la makao makuu ya jeshi la Syria mjini Damascus. Vyanzo viwili vilivyo karibu na idara ya usalama ya Syria vimesema kuwa shambulio la Israeli liliikumba Wizara ya Ulinzi huko Damascus.

Jana, Jumanne, Julai 15, mwanadiplomasia wa Marekani, Tom Barrack, alielezea ghasia mbaya katika jimbo la Sweida kuwa "zinazotia wasiwasi" na kusisitiza kuwa serikali yake inajitahidi kurejesha hali ya utulivu nchini humo. "Mapigano ya hivi majuzi huko Sweida yanatia wasiwasi pande zote, na tunajitahidi kufikia matokeo ya amani na shirikishi kwa makabila ya Druze na Bedouin, serikali ya Syria, na vikosi vya Israeli," Tom Barrack, mjumbe maalum wa Washington nchini Syria, amesema kwenye mtandao wa kijamii wa  X, akinuku pande zinazohusika katika ghasia tangu siku ya Jumapili.

Israel inafanya kazi kama mlinzi wa Druze na kwa maslahi yake binafsi, anasisitiza mwandishi wetu wa Jerusalem, Michel Paul. Ikumbukwe kuwa kuna ushirikiano wa kina na Druze wa Israel wanaohudumu katika jeshi la Israeli. Tofauti na Waarabu wengine wa Israeli, Druze wako chini ya uandikishaji wa lazima wa kijeshi. Hali ni ya kutatanisha zaidi kuhusu jamii ya Druze katika milima ya Golan, iliyotwaliwa na Israel. Kuhusu washiriki wa jumuiya hii wanaoishi Syria, wamegawanyika sana kuhusu uhusiano wao na Israeli. Ikumbukwe kwamba Wadruze ni kundi la watu zaidi ya milioni moja ambao, ingawa wametawanyika kijiografia kati ya Israeli, Lebanoni, na Syria, wameunganishwa na utamaduni na dini—tofauti ya Ushia—ambayo inawaunganisha pamoja. Jamii haikubali waongofu wapya na inakatisha tamaa ndoa nje ya jumuiya, wataalamu wanaripoti.

Siku chache tu zilizopita, kulikuwa na mazungumzo ya mawasiliano kati ya Israeli na Rais mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kwa lengo la hatimaye kuhalalisha kati ya nchi hizo mbili. Jumanne, Julai 15, waziri wa Israeli alitoa wito moja kwa moja aondolewe, akimtaja kuwa gaidi na muuaji mkatili. Leo Jumatano, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Marekani iliitaka Israel kusitisha mashambulizi yake ya anga nchini Syria. Ombi ambalo linaweza kuwa ngumu kwa Israeli kukataa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii