Jera miaka 20 kwa udhalilishaji wa kingono

Mkazi wa Kijiji cha Lituhi kilichopo Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma Winfridi Twahibu Mahundi {29} amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la udhalilishaji wa kingono kwa mtoto wa miaka 03.

Hukumu hiyo imesomwa juni 23.2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa Mhe Osmund Nsackhatu Ngatunga ambapo amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 04/06/2025 katika kijiji cha Lituhi, wilayani Nyasa ambapo alimchukua mhanga na kumpeleka kwenye jengo bovu ambamo alimvua nguo na kumchezea sehemu zake za siri kwa mkono na baadae kumvalisha nguo na kumtelekeza nje ya jengo hilo kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali Frank Sarwatt na Mwendesha mashtaka Wilaya ya Nyasa Hope Milanzi wamesema kuwa mshatakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo tarehe 23.06.2025 na kusomewa shtaka la udhalilishaji wa kingono kwa mtoto mwenye umri wa miaka 03, ambapo mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo na alikubali hoja zote zilizotolewa na upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka ulitoa vielelezo vitatu mahakamani hapo na Mahakama ilijiridhisha kwamba upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo pasi na kuacha shaka dhidi ya mshtakiwa.

Mshtakiwa katika utetezi wake aliiomba mahakama imuhurumie maana ni mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo na ana ndugu wanaomtegemea.

Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali utetezi wa mshakiwa na kumuhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 20 jela na fidia ya Tshs 500,000/= kwa mhanga.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii