Waasi wa Congo na M23 kuanza mazungumzo nchini Qatar kwa shinikizo la Trump

Serikali ya Kongo na waasi wa M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, wametangaza siku ya Alhamisi kurejea kwa wajumbe wao nchini Qatar kwa mazungumzo ya amani, wakati Washington inataka kukomesha mapigano, ambayo yanaweza kufungua mabilioni ya dola katika uwekezaji wa madini.

M23 inashikilia eneo kubwa zaidi kuliko hapo awali mashariki mwa Kongo baada ya kusonga mbele mapema mwaka huu. Mapigano, ambayo ni machafuko ya hivi punde zaidi katika mzozo ambao chimbuko lake ni mauaji ya halaiki ya Rwanda miaka 30 iliyopita, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine mamia ya maelfu kuyahama makazi yao.

Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unajaribu kusuluhisha mkataba wa amani kati ya Rwanda na Kongo ambao utavutia mabilioni ya dola katika uwekezaji wa nchi za Magharibi katika eneo lenye utajiri wa tantalum, dhahabu, kobalti, shaba, lithiamu na madini mengine. 

Qatar inaendesha upatanishi tofauti lakini sambamba na wajumbe kutoka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na M23. Wiki iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo walitia saini makubaliano ya amani mjini Washington, wakijitolea kutekeleza makubaliano ya mwaka 2024 ambayo yanataka kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda mashariki mwa Kongo ndani ya siku 90.

Wanadiplomasia hao wakuu pia walikutana na Trump, ambaye alimwalika Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame mjini Washington kutia saini makubaliano ambayo Massad Boulos, mshauri mkuu wa Trump barani Afrika, aliyapa jina la "Mkataba wa Washington."

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, Boulos alisema utawala wa Trump "utafurahi" kufanya mkutano huo mwishoni mwa mwezi wa Julai. Pia aliongeza kuwa maafisa wa Marekani wanatumai kuwa makubaliano yatakamilika huko Doha kufikia wakati huo. 

Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, mkutano wao wa kwanza tangu kutiwa saini kwenye mkataba wa kihistoria wa amani, wiki iliyopita mjini Washington, afisa wa M23 amesema wajumbe wa waasi watarejea Doha, lakini akaishutumu Kinshasa kwa kutochukulia mchakato huo kwa uzito.

Waasi wanaendelea kusisitiza juu ya maendeleo ya masharti kama vile kuachiliwa kwa wapiganaji wa M23 wanaozuiliwa na kufunguliwa tena kwa benki katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, ameongeza.

Ofisi ya rais wa Kongo imesema katika taarifa yake kwa shirika la habari la REUTERS kwamba wajumbe wa serikali pia wanarejea Doha. Ripoti ya hivi punde kutoka kwa jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa, iliyopatikana wiki hii na REUTERS, inaonyesha kuwa Rwanda ilitumia maagizo na udhibiti wa M23 wakati operesheni zake.

Rwanda imekanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa M23, na msemaji wa serikali alisema wiki hii kwamba ripoti hiyo "inawakilisha vibaya wasiwasi wa muda mrefu wa usalama wa Rwanda" mashariki mwa Kongo, pamoja na uwepo wa wanamgambo wa Kihutu wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Licha ya vikwazo vilivyosalia vya kumaliza mzozo huo uliodumu kwa muda mrefu, Boulos alisema Jumatano ana "matumaini" kwamba Tshisekedi na Kagame wako tayari katika kufikia makubaliano.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii