WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) kwa kuahidi kutekeleza miradi mipya katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya kilimo na pia kuwawezesha Wanawake na Vijana kiuchumi pamoja
na ahadi aliyoitoa ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya
Kisasa-SGR
Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo Jijini Dodoma,
alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki hiyo, Dkt. Akinwumi
Adesina, akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.
Alisema kuwa Benki
hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko za jijini
Dodoma pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Msalato utakaojengwa
mkoani Dodoma, miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amemshukuru
Rais huyo wa Benki ya AfDB kwa nia ya kusaidia miradi mingine mipya
kama ya Uwezeshaji wa Wanawake na vijana lakini pia uwezeshaji katika
sekta kuu za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo.
Amesema maeneo
hayo ni muhimu katika kukuza uchumi na yanamatokeo chanya si tu kwa
watanzania lakini pia kwa Bara la Afrika kwa kuwa mradi kama wa Reli
utazinufaisha nchi Jirani kwa kuwa Tanzania ina lango la Bahari hivyo
miundombinu hiyo itasaidia katika kuchochea uchumi wa nchi hizo Jirani
na nyingine.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameipongeza Benki hiyo kwa
utendaji kazi mahili chini ya Rais Dkt. Akinwumi Adesina, kwa kuwa mwaka
2021 ilitunukiwa tuzo kwa kuwa Benki Bora Duniani katika masuala ya
Fedha na pia ameshukuru kwa nia ya kusaidia utekelezaji wa miradi mipya
ambayo itawasaidia watanzania.
Kwa upande wake Rais wa AfDB,
Dkt. Akinwumi Adesina alisema kuwa Benki yake inatambua umahili wa
Tanzania katika kusimamia sera za kifedha na kiuchumi na kuahidi kuwa
Benki yake itaendelea kuchangia maendeleo yake katika Nyanja mbalmbai
ikiwemo miundombinu ya nishati na barabara, kilimo, uhifadhi wa
mazingira, pamoja na kuendeleza sekta binafsi.
Dkt. Adesina
alisema kuwa uwekezaji wa Benki yake katika miradi mbalimbali ya kijamii
na kiuchumi hapa nchini umefikia dola za kimarekani bilioni 2.5 na
kwamba Benki yake iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mipya hususani katika sekta ya kilimo ili nchi iweze kuzalisha
chakula kwa wingi na kukiongezea thamani kupitia maeneo maalumu ya
uwekezaji.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu na Mlipaji
Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki
hiyo kwa baadhi ya nchi za Afrika, Bw. Amos Cheptoo pamoja na Kaimu
Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduor, ambapo kesho,
Mheshimiwa Dkt. Akinumwi anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.