Shirika lisilo la kiserikali la Hostage Aid Worldwide limetangaza siku ya Jumanne Desemba 24, 2024 mjini Damascus kwamba askofu, raia wa Syria mwenye asili ya Marekani, Yohanna Ibrahim, aliyetekwa nyara mwaka 2013 wakati wa vita nchini Syria, alionekana katika jela chini ya mamlaka ya Bashar Al Assad miaka mitano baadaye.
“Yohanna Ibrahim ni raia wa Marekani. Alionekana mwaka wa 2018 idara ya 291, gereza la Damascus, amesema Nizar Zakka, kiongozi wa shirika hilo.
Mkuu wa Dayosisi ya Othodoksi ya Aleppo huko syria (kaskazini) alitekwa nyara pamoja na Boulos Yazigi, mkuu wa dayosisi ya Othodoksi ya Ugiriki ya jiji hilo, mwezi wa Aprili 2013 karibu na Aleppo. Utawala wa Syria ulinyooshea kidole cha lawama "wanajihadi wa Chechnya" kwa kumteka nyara kiongozi huyo wa kidini.
Wakati huo huo shirika lisilo la kiserikali la Hostage Aid Worldwide limetangaza Jumanne hii mjini Damascus kwamba liko na "data" ambazo zinonyesha kwamba mwandishi wa Marekani Austin Tice, aliyetoweka nchini Syria tangu 2012, " yuko hai". "Tuna data kwamba Austin alikuwa hai hadi Januari 2024, na Rais wa Marekani alisema mnamo Agosti kwamba yu hai, na tuna imani kuwa yuko hai leo," amesema Nizar Zakka, rais wa shirika hili ambalo linafanya kazi na familia ili kuwaachilia raia waliotekwa nyara.