Wizara ya Afya ya Urusi imetangaza kuwa imegundua chanjo dhidi ya saratani ambayo itatolewa bure kwa wagonjwa na inatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwaka 2025.
Andrey Kaprin, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Tiba ya Mionzi cha Wizara ya Afya nchini Urusi, alisema chanjo hiyo itazinduliwa mwanzoni mwa 2025.
Inaelezwa kuwa chanjo hiyo itatumika pia kuwatibu wagonjwa wa saratani na itatolewa bure kwa wananchi ili kuipa miili yao kinga ya kuzuia saratani kabla haijatokea.
Maoni ya awali kutoka kwa wanasayansi wa serikali ya Urusi yanaonyesha kuwa kila chanjo itatengenezwa kwa ajili ya mgonjwa mmoja mmoja, hali inayofanana na chanjo za saratani zinazoendelea kutengenezwa katika nchi za Magharibi.
Mpaka sasa bado Urusi inayoongozwa na Rais Vladmir Putin haijabainisha ni aina gani za saratani ambazo chanjo hiyo inalenga kutibu, ufanisi wake na jinsi itakavyosambazwa.
Jina la chanjo hiyo pia bado halijatangazwa ambapo kama ilivyo sehemu nyingine za dunia, viwango vya saratani vinaongezeka nchini Urusi, huku zaidi ya visa 635,000 vikirekodiwa mwaka wa 2022.
Saratani ya utumbo mpana, saratani ya matiti, na saratani ya mapafu zinaaminika kuwa aina za saratani zilizoenea zaidi nchini humo.