FAMILIA ya mvulana mwenye umri wa miaka 12 aliyepigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali, imeagizwa na mahakama kutafuta mbinu mbadala za kutatua mgogoro baina yao.
Hakimu Mkuu wa Mbita, Nicodemus Moseti, amewaagiza wazazi kuafikiana na kusuluhisha kivyao tofauti kati yao badala ya kuelekea kortini ili mahakama iwatatulie suala hilo. Wazazi, Denish Okinyi na Jocinta Anyango waliotengana, walitofautiana kuhusu eneo la kumzika mwana wao.
Bw Okinyi anataka mvulana huyo azikwe nyumbani kwake katika kijiji cha Kisaku, Kaksingri Magharibi, kaunti ndogo ya Suba.
Naye Bi Anyango, aliyeolewa na mwanamume mwingine, anataka mwanawe azikwe eneo la Kamasengre katika Kisiwa cha Rusinga.
Alikuwa amefanya maandalizi ya mazishi na alipaswa kumzika mwanawe Kennedy, Julai 5,2024, lakini Okinyo akaelekea kortini na kusimamisha mazishi.
Bw Moseti amewataka wazazi hao kuzungumza na kuafikiana kuhusu wanapofaa kumzika mtoto wao.“Mkishindwa kuafikiana, mnaweza kurejea kortini ili mwongozo zaidi utolewe,” alisema Hakimu.
Korti katika Kaunti ya Homa Bay zilianzisha mchakato wa maridhiano ili kupunguza mlundikano wa kesi na kusaidia pande husika kuokoa hela hasa ikiwa inahusu familia.
Katika mchakato wa korti unaohusu maridhiano, wazazi watakutana na mpatanishi atakayewasaidia kutatua suala hilo nje ya mahakama.
Mchakato huo utaanza leo mbele ya naibu msajili anayesimamia maridhiano.
Bw Humphrey Obach, wakili anayemwakilisha Bi Anyango ameelezea wasiwasi wake kuhusu mochari ya Hospitali ya Suba ambapo mwili wa Kennedy umehifadhiwa.