IMF yaidhinisha ufadhili wa dola milioni 900 kwa Tanzania

Shirika la kimataifa la fedha (IMF) Alhamisi limesema bodi yake ya utendaji imeidhinisha ufadhili wa dola milioni 786.2 kwa Tanzania kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Shirika hilo la kifedha linakamilisha pia tathmini tofauti ya kuruhusu malipo ya dola milioni 149.4 kwa ajili ya msaada wa bajeti.

Mamlaka za Tanzania zina dhamira ya kuendelea kutekeleza mageuzi ya kudhibiti uthabiti wa kifedha, kuimarisha ufufuaji wa uchumi, kukuza ukuaji endelevu na shirikishi, IMF ilisema katika taarifa.

Katika miaka mitatu iliyopita, utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ulifanya mageuzi mbalimbali ya kiuchumi kwa lengo la kurudisha ukuaji wa uchumi katika kiwango cha ukuaji wa pato la taifa la kabla ya janga la Covid wa asilimia 6 hadi asilimia 7.

Mpango wa mageuzi ya uchumi wa Tanzania bado umeendelea kuwa imara, IMF imesema, na kuongeza kuwa ukuaji wa uchumi uliongezeka mwaka 2023 baada ya kupungua mwaka 2022.

Uchumi wa Tanzania ambao unategemea utali, madini, kilimo na viwanda, umeendelea kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa yanayochochewa na kuongezeka kwa sekta ya huduma, kulingana na Benki ya Dunia.

Uchumi wa Tanzania unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka huu, kutoka asilimia 5.1, waziri wa mipango na uwekezaji katika Ofisi ya Rais, Kitila Mkumbo alisema wiki iliyopita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii