Boris hataki kutoa majibu mahsusi kutoingilia uchunguzi wa polisi

Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Dominic Raab amesema waziri mkuu wa nchi hiyo, Boris Johnson, hawezi kutoa majibu kamili juu ya dhifa kadhaa zilizofanyika kwenye ofisi yake ya Mtaa wa Downing wakati wa vizuizi vikali vya kukabiliana na Covid-19 kwa sababu hataki kuingilia uchunguzi unaofanywa na polisi. Raab amekiambia kituo cha televisheni cha Sky kuwa iwapo Johnson atatoa majibu kuhusu masuala mahsusi ambayo tayari yanachunguzwa na polisi anaweza kukosolewa kuwa anauweka rehani uchunguzi unaoendelea. Polisi ya Uingereza inapitia karibu nyaraka 500 na zaidi ya picha 300 kama sehemu ya uchunguzi mpana juu ya iwapo ofisi ya waziri mkuu ilivunja sheria kwa kuandaa karamu zilizopigwa marufuku chini ya vizuizi vya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Uchunguzi wa awali kuhusu suala hilo umebaini uzembe katika uongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo na kuongeza shinikizo la kumtaka Johnson kujiuzulu

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii