Wanaharakati nchini Uganda pamoja na wanasiasa nchini humo, wamewakosoa maofisa kadhaa wa juu wa Serikali ya Uingereza, kwa kile wamesema upuuzi kwa maofisa hao kumpongeza mtoto wa rais Yoweri Museveni kuteuliwa kuwa mkuu wa majeshi huku akiwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Gazeti la Uingereza la The Guardian, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alipokea barua ya pongezi kutoka kwa afisa mkuu wa majeshi ya Uingereza, Sir Tony Radakin, ambaye aliambatana na maofisa wengine wajuu wa Serikali katika kikao na kiongozi huyo.
Kainerugaba ameshutumiwa kwa kufadhili ghasia na kuwadhulumu wakosoaji wa Serikali, ambapo baadhi ya wadau walifungua kesi katika mahakama ya ICC, madai ambayo Kainerugaba na baba yake wameyakanusha.
Hata hivyo Amos Katumba, mshirika wa kiongozi wa upinzani Bobi Wine, ambaye anaendesha shirika la kusaidia watoto la Caring Hearts Uganda amesema wamesikitishwa na hatua ya uongozi wa Uingereza.
Kwa upande wake, Andrew Mwenda, msemaji wa Jenerali Kainerugaba, amesema kiongozi wake haamini katika ukiukaji wa haki za binadamu na hivyo hawezi kuhusika katika ukiukwaji wowote wa haki za watu.