Polisi ya Uturuki yawatia mbaroni waandamanaji 200

Polisi wa Uturuki jana Jumatano walifyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira pamoja na kuwaweka kizuizini  zaidi ya waandamanaji 200 baada ya mamlaka kupiga marufuku mikusanyiko ya kuadhimisha ya Mei Mosi iliyopangwa kufanyika katika uwanja wa kihistoria wa taifa hilo wa Taksim huko mjini Istanbul.


Waandishi wa AFP wameripoti kuwa polisi walikabiliana na waandamanaji karibu na ukumbi wa jiji katika wilaya ya Sarachane, wakifyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwazuia waandamanaji kuvunja vizuizi.

Waziri wa mambo ya ndani Ali Yerlikaya aliandika kwenye ukurasa wake wa X, zamani Twitter kwamba, watu 210 wamekamatwa Istanbul kwa kutotiii onyo lao na kuwashambulia polisi siku ya Mei Mosi.

Zaidi ya polisi 40,000 walisambazwa kote Istanbul, wakizuia hata mitaa midogo ya pembeni kwa vizuizi vya chuma katika jaribio la kuzuia waandamanaji kukusanyika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii