Leo ni Siku ya Kimataifa ya Furaha, na kwa mara ya saba mfululizo, nchi ya Finland imetangazwa kuwa nchi ambayo raia wake wana furaha zaidi duniani.
Finland inafuatiwa na majirani zake wa eneo la Nordic ambao ni Sweden, Denmark na Iceland.
Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila mwaka na Umoja wa Mataifa imebaini kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na furaha hasa miongoni mwa vijana katika Mataifa ya Magharibi.
Hilo limepelekea mataifa kama Ujerumani na Marekani kuondolewa katika orodha ya nchi 20 bora zenye furaha duniani na nafasi zao kuchukuliwa na mataifa ya Costa Rica na Kuwait.
Lakini nchi za Ulaya Mashariki kama Serbia, Bulgaria na Latvia ziliripoti ongezeko kubwa la furaha.
Nafasi ya mwisho katika orodha hiyo inashikiliwa na Afghanistan iliyokumbwa na janga la kibinaadamu.