Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu baada ya wiki kadhaa za machafuko yanayoongozwa na magenge ya watu wanaotaka aondolewe madarakani.
Henry alikuwa nchini Kenya kutia saini mkataba wa kutumwa kwa kikosi cha polisi wa kimataifa kusaidia kukabiliana na ghasia wakati makundi wa magenge yaliposhambulia vituo vya polisi na kuvamia magereza mawili makubwa zaidi ya Haiti.
Ndege iliyokuwa imembeba Henry ilizuiwa kutua kufuatia mashambulio ya magenge katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Haiti.
Marekani imetangaza kutoa msaada zaidi wa kifedha kwa Haiti, kufanikisha kikosi cha kimataifa, kitakachoongozwa na polisi kutoka nchini Kenya, kusaidia kukabiliana na magenge yenye silaha, yanayoendelea kusababisha utovu wa usalama nchini humo.
Hili limethibitishwa na Waziri wa Mambo ya Antony Blinken, wakati alipohudhuria kongamano la Kimataifa jijini Kingstone Jamaica, kujadili hali inavyoendelea Haiti.
Haya yanajiri wakati huu serikali ya Kenya ikiwa imesisitiza kuendelea na mpango wake wa kuwatuma maofisa wa polisi nchini Haiti licha ya kuongezeka kwa ghasia za magenge katika nchi hiyo ya Caribbean.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani nchini Kenya Kithure Kindiki hapo jana Jumatatu, mpango wa kutumwa kwa polisi hao elfu moja umefikia katika hatua za mwisho.
Waziri Kindiki pia alisema kuwa sheria za utekelezaji, kama vile kuzuiliwa na kukamatwa, zimekamilika.
Aidha waziri Kindiki alisema kuwa serikali ya Kenya imeshughulikia masuala yote yaliyoibuliwa mahakamani ambayo yalikuwa yamezuia utekelezwaji wa mapngo huo.
Licha ya tangazo hilo la serikali, tarehe kamili ambayo maafisa hao wataondoka nchini nchini Kenya bado haijaekwa wazi.