Dkt. Biteko: Rais Samia hataki misukosuko kwa Wafanyabiashara

Aidha, amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha wanailea Sekta binafsi na kila mtu atimize wajibu wake kwenye eneo lake na kwamba Watendaji ambao ni warasimu lazima waone aibu kwa kuchelewesha shughuli zinazoijenga nchi.

Amesema, “kama wewe ni Afisa wa TANESCO uliye na wajibu wa kumuunganishia mfanyabiashara umeme ambao mwisho wa siku ataulipia kwa ajili ya mapato yako, huna sababu ya kumwambia njoo kesho wakati kazi hiyo ungeifanya leo.”

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka kuona watanzania wakiwa kwenye daraja la kwanza katika nchi yao na pia waweze kufanya uwekezaji ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

Kuhusu Sekta ya Utalii nchini, amesema bado kuna changamoto ya upungufu wa vitanda kwa wageni wa ndani na nje ya nchi hivyo bado kuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya ‘hospitality’ ambapo amewapongeza wamiliki wa Rafiki hoteli na wawekezaji wengine ambao wanaifanyia kazi changamoto hiyo.

Dkt. Biteko pia ameipongeza menejimenti ya hoteli hiyo kwa kutekeleza dhana ya nishati safi ya kupikia kutokana na kuweka miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye hoteli husika na kutoa wito kwa wananchi kutoharibu mazingira na kutokukata miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu Idara na taasisi mbalimbali Serikalini kutumia miundombinu ya uwekezaji Jijini Dodoma ambayo ndio Makao Makuu ya Nchi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii