Mwandishi wa Kimarekani aendelea kushikiliwa Urusi

Mahakama moja nchini Urusi imeongeza muda wa kuzuiliwa hadi mwisho wa mwezi Machi kwa mwandishi wa gazeti la Wall Street Journal la Marekani, Evan Gershkovich, aliyekamatwa kwa tuhuma za ujasusi.

Balozi wa Marekani nchini Urusi, Stuart Wilson, alihudhuria kikao hicho, kilichofanyika faraghani kwa sababu mamlaka ya Urusi kueleza kuwa kesi ya jinai dhidi ya mwandishi huyo wa habari wa Marekani ni siri ya serikali.

Katika vidio iliyotolewa na shirika la habari la Ria Novosti, Evan Gershkovich alionekana akisikiliza kesi hiyo mahakamani na baada ya uamuzi huo kutolewa, alipanda gari la kubebea wafungwa na kuondoka mahakamani. 

Gershkovich, mwenye umri wa miaka 32, alikamatwa mwezi Machi katika mji wa Yekaterinburg, karibu kilomita 2,000 mashariki mwa Moscow.

Mamlaka za Urusi zinamtuhumu mwandishi huyo kwa kukusanya habari juu ya jeshi la Urusi kwa niaba ya Marekani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii