Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven
Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wakubwa wa
madini ya Vito ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wachimbaji wa
madini kupata Masoko.
Hayo yameelezwa alipotembelea machimbo ya migodi ya Vito (Ruby) katika Kata ya Mundarara wilayani Longido Mkoa wa Arusha.
Agizo
hilo, amelitoa alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo
hilo baada ya kupokea malalamiko ya wachimbaji hao kukosa soko la
uhakika la Madini aina ya Vito hususan yenye ubora wa kati na hafifu
(Semi Gem/Cheapstone) yanayopatikana kwa wingi katika mkoa wa Arusha.
Pia,
aliendelea kusema Serikali imebaini wapo watu wanafanya shughuli za
uchimbaji madini ambao hawapo kwenye mfumo rasmi na hawana leseni wala
kitalu lakini wanajishughilisha na masuala ya madini kiholela na
kupelekea hasara kwa Taifa.
Vile vile, alisema Serikali ipo
kwenye hatua ya kutambua aina ya Madini yote yanayochimbwa nchini katika
maeneo mbalimbali pamoja na kubaini maeneo mapya yenye madini ili
Serikali inufaike, amesema taasisi zipo mbili, GST hupima juu ya Ardhi
na kubaini madini yaliyopo pamoja na STAMICO wanaofanya tafiti za nadini
kwa kwenda chini zaidi.
Naye, Kamishina wa Madini Dkt
Abdulrahman Mwanga amesema miradi ya kimkakati ni muhimu ili wananchi
waweze kunufaika na huduma za kijamii, hivyo amewataka wawekezaji hao
kujitahidi kushirikiana na wananchi katika kutekeleza miradi mbalimbali.
"Wawekezaji
wanapaswa kutekeleza wajibu na matakwa ya Sheria katika kuendeleza
maeneo yao ili kupunguza migogoro inayojitokeza na Wananchi"alisema Dkt
Mwanga
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurudin Babu aliwaasa
wachimbaji hao kufanya kazi kwa kushirikiana na kuepuka mikwaruzano,na
matatizo yatakayojitokeza ni vyema yakatolewa taarifa kwake kabla
hayajafika kwa Naibu Waziri.
Ofisa Madini Mkoa wa Arusha,
Mhandisi Alphonce Rikulamchu amesema uwepo wa madini aina mbalimbali
katika wilaya ya Longido ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa wilaya
na Watanzania wote kwa ujumla.
Mhandidsi Rikulamchu ametoa wito
kwa wachimbaji , wafanyabiashara ya madini na wadau wote kuendelea
kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu ili
kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato stahiki ya
Serikali.
Mmiliki wa kampuni ya Sendeu Agrovet Co. Ltd
inayomilikiwa na mwekezaji mzawa Gabriel Sendeu alisema kazi ya
uzalishaji inaendelea katika mgodi huo na kueleza kuwa mgodi huu kwa
Sasa ni kitovu cha mapato ya Serikali.
" Kampuni yetu imekua
ikisaidia miaka yote kusomesha watoto yatima, hii ni baraka naomba na
wengine wenye uwezo tusaidie watoto hao waliopo ndani ya jamii", alidai
Sendeu.
Wilaya ya Longido ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa
Arusha iliyojaliwa kuwa na madini ya Vito (Ruby, Spessartite, Sunstone
na Quartz) katika maeneo ya Sinonik, Kimwati na Mundarara pamoja na
Madini ujenzi mchanga.