Umoja wa Mataifa umesema Mkuu wa jeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na mpinzani wake, aliyeongoza kundi la RSF Mohamed Hamdan Daglo, wamekubali kukutana kwa ajili ya mazungumzo kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya binadamu Martin Griffiths amesema siku chache zilizopita, alizungumza na viongozi hao wawili lakini haijathibitishwa ni lini na wapi mazungumzo hayo yatafanyika.
Taarifa hii inakuja wakati huu Umoja wa Mataifa ukiomba msaada wa Dola Bilioni 4.1 kuwaisaidia mamilioni ya watu ambao wameathiriwa na vita vilivyoanza mwezi Aprii mwaka uliopita.
Watu Milioni 25 karibu nusu ya watu nchini Sudan wanahitaji msaada wa chakula, dawa na makaazi baada ya kuyakimbia makaazi yao.
Watu wengine Milioni 1.5 ambao pia wamekimbilia katika nchi jirani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wanahitaji pia msaada wa haraka.