Huenda Urusi ikawatuma wanajeshi wake Burkina Faso: Ibrahim Traore

Nairobi – Kiongozi wa kijeshi nchini Burkina Faso amesema nchi ya Urusi huenda ikawatuma wanajeshi wake nchini mwake kusaidia katika vita dhidi ya makundi ya wanajihadi iwapo hatua hiyo itastahili kuchukuliwa.

Ibrahim Traore -Kiongozi wa kijeshi nchini Burkina Faso
Ibrahim Traore -Kiongozi wa kijeshi nchini Burkina Faso © Capture d'écran/le MondeAfrique.fr/ AFP
MATANGAZO YA KIBIASHARA

Ibrahim Traore ameeleza kuwa Urusi kwa sasa inatoa mafunzo ya kimkakati na iko tayari kuiizuia nchi yake silaha inazohitaji.

Aidha kiongozi huyo wa kijeshi ameeleza kuwa hakuna vikwazo kuhusu ni nini ambacho nchi yake haistahili kununua kutoka kwa mataifa ya China, Urusi, Uturuki na Iran ikilinganishwa na nchi zengine.

Matamshi yake yanakuja wakati huu kukiwepo na ripoti kwamba karibia wapiganaji wa Urusi mia moja walitumwa kwenye taifa hilo la Afrika wiki iliopita kutoa mafunzo ya kijeshi.

Matukio hayo yanaibua madai kwamba Burkina Faso inataka kuimarisha uhusiano kiusalama na nchi ya Urusi kama ilivyo kwa nchi jirani ya Mali, ambako mamluki wa Wagner wa Urusi wanafanya kazi.

Uhusiano kati ya mataifa yanayoongozwa na jeshi barani Afrika na Moscow umeonekana kuimarika tangu mapinduzi ya kijeshi yalipotokea kwenye mataifa hayo.

Burkina Faso imekuwa ikipambana na makundi ya kiislamu yenye mafungamano na al-Qaeda na Islamic State, ambayo yamechukua maeneo kadhaa ya nchi.