Tanzania yatakiwa kupunguza gharama za utalii wa ndani

Gharama za utalii na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa utalii unasababisha utalii wa ndani kuwa chini wakati Tanzania inapokea watalii wengi kutoka mataifa ya kigeni.

Hayo yamesemwa na baadhi ya wadau wa utalii na wananchi siku ya Jumatano wakati wa Tanzania inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kimataifa ya utalii duniani.

Wamesema mbali sekta hiyo inaonyesha mafanikio, watanzania wengi hawana elimu kuhusu utalii, hivyo wameitaka serikali kutoa elimu zaidi pamoja na kupunguza gharama za viingilio, malazi na usafiri ndani ya hifadhi ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kutembelea maeneo hayo.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Profesa Winiesta Anderson kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema serikali inatakiwa kutoa elimu na kuweka utalii wa ndani kama somo linaloanzia shule za msingi ili kulenga utamaduni wa Watanzania katika kufanya utalii ambao utaongeza mapato kwa serikali.

“Tuendelee kuutangaza utalii lakini tuendelee kulifanya ni somo kwa mfano kuanzisha zile safari za kutembelea maeneo ya utalii kwa wanafunzi katika shule za msingi katika shule za sekondari.” Alisema Anderson.

Licha ya ongezeko la watalii wa ndani kutoka watalii 700,000 mwaka 2021 hadi kufikia watalii million 2.4 mwaka 2022 ambayo ni sawa na asilimia 199.5 lakini bado ongezeko hilo ni dogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania.

Suala ambalo wananchi wamedai linachangiwa na gharama za usafiri na malazi ndani ya vivutio vya utalii, na kuwafanya washindwe kutembelea vivutio hivyo.

Hussein Kinoko, mtanzania anayezungumzia gharama za usafiri na malazi alisema “kizaa zaa kinakuja kwenye gharama za malazi na usafiri unapofika Ngorongoro au Serengeti ni rahisi kiingilio kipo chini ya shillingi elfu ishirini kwa Mtanzania” na kuongeza “lakini ni ngumu sana kupata lile gari kwa siku ni zaidi ya shillingi laki mbili wengine wanafika mpaka zaidi ya shilingi laki tatu hiyo inatuwia ugumu sana kuingia kwenye hivi vivutio”

Hata hivyo Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki aliiambia Sauati ya Amerika kuwa mpango wa serikali ni kuendelea kutangaza utalii wa ndani na kupunguza gharama hizo ili kuwawezesha Watanzania kufanya utalii wa ndani.

“lakini tunajua bado tunahitaji kuendelea kupunguza zaidi gharama kwahiyo tunaendelea kufanya mapitio ya gharama zetu kwa kushirikiana na wadau wetu katika sekta yetu ya utalii ili kuhakikisha kwamba kwa kiasi kikubwa wananchi wetu na wenyewe pia wanaweza kutumia vivutio vyao vya ndani nakuweza pia kutalii.” Alisema waziri huyo wa Utalii.

Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani mwaka 2023 yamebeba kauli mbiu inayosema "Utalii na Uwekezaji wa Kijani." Msisitizo ukiwa umuhimu wa utalii endelevu ambao unazingatia mazingira na uchumi wa kijani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii